DRC. Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) imekemea matumizi ya silaha za maangamizi, zikiwemo ndege zisizo na rubani za mashambulizi, ambazo inadai zimekuwa zikilenga raia katika maeneo mbalimbali ya Mashariki mwa nchi hiyo.
Serikali imesema mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu takribani 100, kujeruhi maelfu na wengine zaidi 200,000 kuhama makazi yao katika kipindi cha hivi karibuni tangu yatokee machafuko
Tovuti ya BBC Swahili imeeleza kuwa, Msemaji wa Serikali Patrick Muyaya amesema mashambulizi hayo yameathiri maeneo ya mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini na yanachukuliwa kama uvunjaji wa makusudi wa makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na Makubaliano ya Washington yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Muyaya alionya kuwa hali hiyo ni tishio kwa uthabiti wa Jumuiya ya Maziwa Makuu.
Amesema kuwa kulenga pia nchi jirani ya Burundi baada ya mashambulizi hayo ni jaribio la kuisambaratisha na kuichanganya kanda nzima, akisisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuzingatia na kuweka vikwazo dhidi ya wahusika wanaokiuka makubaliano ya amani.
Serikali ya DRC imesisitiza kuwa inachukua hatua kupitia mamlaka za kitaifa na za Mkoa wa Kivu Kusini kukomesha mashambulizi hayo, huku ikitoa wito kwa wananchi kuungana na kuonyesha mshikamano wa kitaifa katika kukabiliana na kile inachokitaja kuwa uvamizi.
Hata hivyo, Rwanda kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imekanusha kwa mara nyingine kuhusika na mashambulizi au uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ikisema shutuma hizo hazina msingi.
Mivutano kati ya Kinshasa na Kigali imeendelea katika kipindi cha mwaka uliopita, huku mashambulizi ya silaha nzito na ndege zisizo na rubani yakiendelea kuvuruga hali ya usalama Mashariki mwa DRC na kusababisha kadhia kwa wananchi.
