SIMBA Jumapili ya Desemba 7, 2025 ilikubali kipigo cha kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Azam, lakini mabosi wa klabu hiyo tayari wamepanga kupitisha panga kwa mastaa watatu wa kigeni, huku pia mchakato wa kusaka kocha mpya ukiendelea baada ya kuondoka Dimitar Pantev.
Panga hilo limepangwa kupita katika dirisha dogo litakalofunguliwa Januari Mosi, 2026, ikiwa na lengo la kuruhusu kuingiza mashine mpya ili kuipa nguvu kwa mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazoendelea baada ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Mwanaspoti imepata taarifa kwamba kuna majina matatu ya mastaa wa kigeni yaliyowekwa mezani na kuanza kujadiliwa ili kuyakata katika usajili wa dirisha dogo.
Taarifa hizo za ndani kutoka kwa mmoja wa kiongozi wa klabu hiyo zinasema, mbali na majina hayo matatu ambayo kila moja kuna sababu ya mapendekezo ya kutemwa, pia mwingine mmoja anapigiwaΒ hesabu kuuzwa ili kutoa nafasi zaidi kwa wageni wapya kutua Msimbazi.
Kigogo huyo wa Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina amewataja mastaa walio mezani ni kiungo mshambuliaji, Neo Maema aliyejiunga na klabu hiyo msimu huu akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miezi sita uliokuwa na kipengele cha kumuongezea endapo angeonyesha kiwango cha juu, lakini haijawa hivyo.
βViongozi wenye jukumu la usajili wamewasiliana na viongozi wa Maema, hivyo kuna asilimia kubwa asiwe sehemu ya timu kwa sababu hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa. Mbali na huyo pia kuna uwezekano wa kuachana na beki Rushine De Reuck aliyefunga mabao mawili ya Ligi Kuu, lengo ni kusaka mbadala atakayekuwa na kiwango cha juu,β amesema kiongozi huyo.
Mbali na Maema na Rushine, wengine ambao majina yao yanatajwa ni Joshua Mutale ikielezwa licha ya kumpa nafasi ameshindwa kuonyesha kiwango cha kuibeba timu hiyo.
βIlibakia kidogo kuachana naye usajili uliyopita, akaja akafanya vizuri mechi za mwisho hasa za Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo akapewa nafasi, lakini ni kama ameshindwa kuendana na kile ambacho Simba inataka kutoka kwake,β amesema kiongozi huyo na kuongeza:
βPia kuna Steven MukwalaΒ japo alimaliza msimu uliopita na mabao 13 na asisti tatu katika Ligi Kuu, kwa msimu huu hajawa vizuri, hivyo anatafutwa mshambuliaji mwingine akipatikana basi atapewa mkono wa kwa heri, kwani kuna dili la kuuzwa likitiki itakuwa vyema, japo ukiachana na hao, linatarajiwa kutapitisha fagio kubwa kikosini.β
Kuhusiana na usajili mpya kabla ya kusitishiwa mkataba Desemba 2, 2025 aliyekuwa kocha wa Simba japo alitambulishwa kama meneja mkuu, Dimitar Pantev alikaririwa akisema; βSimba ina malengo makubwa, hivyo inatakiwa kusajili wachezajiΒ watakaoendana ya klabu, kwa maana ya kupata wachezaji wa viwango vya juu. Katika dirisha dogo kuna usajili utafanyika kwa kuondoa baadhi ya waliopo sasa.β
Hata hivyo, kabla ya kutekeleza hilo, fagio likapita naye kutokana na kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi D.
Ilianza kwa kipigo cha 1-0 nyumbani mbele ya Petro Atletico ya Angola kisha kulala 2-1 ugenini kwa Stade Malien ya Mali.
Akizungumzia suala hilo, staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel βBatgolβ kwanza alitoa maoni yake juu ya mwenendo wa klabu hiyo akisema Simba inahitaji mabadiliko ili kuifanya ipate matokeo na kuwapa raha mashabiki.
βViongozi wa Simba wajitafakari sana, hali wanayoenda nayo kwa sasa sio nzuri. Mashabiki wanahitaji furaha na si karaha au kunyimwa amani kwa muda mrefu, matokeo mabovu yanapunguza msisimko wa kuishabikia timu na wachezaji wakikosa sapoti sio kitu kizur,β amesema Gabriel.
Katika Ligi Kuu Bara, Simba imecheza mechi tano, imeshinda nne na kupoteza moja dhidi ya Azam kwa mabao 2-0.
Matokeo ya mechi hizo yameifanya Simba kuvuna pointi 12 ikiwa nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikifunga mabao 11 na kufungwa mawili na kwa sasa ligi hiyo imesimama hadi Januari 21, 2025, wakati Simba ikiingia mwaka kwa kucheza mechi za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kuvaana na Esperance ya Tunisia kwa mechi mbili mfululizo.
