Wananchi, CCM wanavyomlilia Jenista Mhagama Peramiho

Songea. Huzuni na vilio vimetawala kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma kutokana na mbunge wao, Jenista Mhagama kufariki dunia leo Alhamisi Desemba 11,2025 jijini Dodoma.

Wananchi hao wamesema wamepokea kwa masikitiko kifo cha Mhagama, huku wengine wakisema taarifa hiyo imewachanganya kwa sababu mbunge huyo alikuwa kiongozi hodari, mzalendo na mchapakazi.

Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Desemba 11,2025 wakazi hao wa Peramiho wameumizwa na kifo cha Mhagama ambaye watakumbuka kwa namna alivyokuwa mstari wa mbele kupigania miradi ya maendeleo ili itekelezwe jimboni humo, kwa manufaa ya wananchi.

Donald Ngonyani anayeishi Peramiho A, amesema jimbo hilo limepoteza malkia aliyejitoa kupeleka maendeleo kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya shule, maghala ya mahindi, stendi, masoko na mafunzo ya kuwajengea uwezo wananchi kwenye kilimo na ujasiriamali.

“Tupeane pole wananchi wenzangu wa Peramiho na Watanzania wote. Tulimpenda Jenista alikuwa kiongozi, amemaliza kazi tumuombee apumzike kwa amani japo pengo lake ni gumu kuzibika,” amesema Ngonyani.

Kwa upande wake, Isabel Haule amesema Mhagama aliungana na Ngonyani kueleza kuwa Mhagama alikuwa mstari wa mbele kupiga maendelo ikiwemo upatikanaji wa barabara za kiwango cha lami na Hospitali ya Wilaya ya Songeni Vijijini.

Kwa mujibu wa Isabel, Mhagama alikuwa mwanasiasa hodari ambaye hakubagua katika kuhudumia wananchi wa jimbo hilo, bali alijishusha kwa kila mtu na kusikiliza kero zinazowakabili.

Mkazi wa Matomondo Songea, Idan Paul amesema Mhagama alikuwa kioo cha jamii aliyewapenda wapiga kura wake na kujitoa kusaidia makundi ya wanawake, wazee na Watoto.

“Nitamkumbuka kwa vitu vingi ikiwemo unyenyekevu wake, mpenda maendeleo kwani alijitoa kwa hali na mali kusaidia wapiga kura. Lakini nitamkumbuka kwa miradi ya mabwawa ya samaki, ng’ombe  wa maziwa na mbolea hakika alitutendea haki,” amesema Aidan.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Mohammed Ally amesema wamechanganyikiwa baada ya kupata taarifa za Mhagama kwa sababu alikuwa kiongozi mkoani humo.

“Tumepata pigo kubwa, tumechanganyikiwa, tumesikitishwa kifo cha Mhagama, tumejipanga kumpumzisha kiongozi mwenzetu.Tutatoa taarifa zaidi kwa sasa hatuna la kuongea zaidi tunamuombea apumzike kwa amani,” amesema Ally.

Mhagama amekuwa mbunge wa Peramiho kuanzia mwaka 2005. Katika kipindi hicho, amekuwa waziri wa wizara mbalimbali katika utawala wa awamu ya nne ya Jakaya Kikwete  awamu ya tano ya John Magufuli na awamu ya sasa ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.