Watoto watakaozaliwa kuanzia 2026 kuingia kundi jipya ‘Kizazi Beta’

Wanasayansi na wataalamu wa masuala ya malezi wamelitaja kundi jipya la watoto watakaozaliwa kuanzia mwaka 2026 kuitwa ‘Kizazi Beta’ (Beta Generation). 

Sababu za kundi hilo kuitwa kizazi Beta ni kutokana na mwendelezo wao wa kile kilichozaliwa miaka ya 2000 cha Alpha, ambacho kilianzisha mapinduzi ya teknolojia na sasa kuendeleza mapinduzi hayo yaliyoingia katika mfumo wa Akili Mnemba na fedha kidigitali.

Hivyo wazazi ambao wanatarajia kupata watoto kuanzia mwakani watahesabika kuwa  sehemu ya Kizazi Beta.

 Kizazi hicho kipya kinachotarajiwa kudumu hadi mwaka 2039.

Mtandao wa netmums.com unadokeza mambo muhimu ambayo jamii na wazazi wanapaswa kutambua sifa bainifu ambazo zitaambatana na watoto wa kizazi beta.

Ingawa jina hili bado ni la majaribio, wanasayansi wameshaanza kutumia istilahi ya Kizazi Beta wakimaanisha watoto wa kizazi kijacho cha mwendelezo wa sayansi na teknolojia.

Jina kizazi beta  linafuata mtindo wa kutumia alfabeti ya Kigiriki, kama ilivyokuwa kwa Kizazi Alpha. Alpha likimaanisha mwanzo wa enzi mpya na sasa Beta linafuata kama mwendelezo wake. Katika sayansi, neno Beta pia hurejelea kitu kilicho kwenye hatua ya majaribio, kinachokua na kubadilika kwa kasi.

Watoto hao watakaozaliwa kuanzia mwakani watakuwa sehemu ya Kizazi Beta ambapo wazazi ni muhimu kufahamu mambo yanayowahusu.

Kizazi hiki kipya kinatajwa kitaishi katika dunia iliyoendelea zaidi kiteknolojia, kijamii na kisayansi.

Kizazi Beta kitazaliwa kati ya mwaka 2026 hadi 2039, kikitanguliwa na Kizazi Alpha (2010–2025) na kinatarajiwa kubadili kabisa namna watoto wanavyoishi na kukua. 

Watoto wa Kizazi Beta watakuwa wakizungukwa na wenzao wa kisasa wa kutumia AI (Akili Bandia), matumizi ya fedha kidijitali na wenye kuzingatia uhalisia na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia. 

Kizazi hiki kitaathiriwa na mageuzi ya haraka ya kiteknolojia, kimazingira na kijamii, jambo linaloweza kuleta changamoto pia fursa nyingi kwao.

Kila mtu ni sehemu ya kizazi fulani na kizazi tunachotoka huonyesha kwa kiasi kikubwa sisi ni kina nani.

Ikiwa ulizaliwa kati ya 1965 na 1980, wewe ni Kizazi X (Gen X). 

Waliozaliwa kati ya 1981 na 1996 ni Millennials. 

Waliozaliwa kati ya 1997 na 2009 ni Kizazi Z (Gen Z). 

Kizazi Alpha (2010–2025) ndicho cha kwanza kuishi kikamilifu katika dunia ya kidijitali.

Kumekuwa na athari chanya na hasi hasa katika Bara la Afrika kutoka kwa kizazi cha GenZ ambacho kimekuwa na mchango tofauti katika nyanja mbalimbali.

Katika masuala ya kijamii kizazi hicho kimekuwa na mchango katika kutaka maendeleo yenye kasi ili kuyakabili maisha ya kila siku.

Pia, katika nchi za Afrika imeshuhudiwa athari hasi na chanya za Gen Z wakitaka mabadiliko ya kiutawala na mifumo.

Pia, Gen Z wanatajwa wamekuwa kichocheo kikubwa kuongezeka shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa njia ya mtandao.