Chongolo: Miradi yote ya umwagiliaji itakamilika, Tume mjipange

Mtwara. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema Serikali itakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilika na kuleta tija kwa wakulima hali itakayoimarisha uchumi na kuleta uhakika wa chakula

Chongolo amesema hayo leo Ijumaa, Desemba 12, 2025 wakati wa ziara yake katika mradi wa mmwagiliaji uliopo wilayani Masasi, mkoani Mtwara unaotekelezwa eneo la Ndanda na Tume ya Umwagiliaji.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji na uchimbaji wa mifereji mirefu na ukikamilika unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 700 kutoka vijiji saba.

“Serikali itahakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilika na kuleta tija kwa wakulima hali itakayoimarisha uchumi na kuleta uhakika wa chakula,” amesema Chongolo.

Amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa bwawa hilo ambalo litachochea matumaini mapya kwa wakulima wa Mtwara kwa kuwawezesha kulima mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mpunga, mahindi na mazao mengineyo.

Chongolo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM amesema ingawa Mtwara inasifika kwa kilimo cha korosho, serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanzisha miradi ya umwagiliaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha uzalishaji wa mazao mengine ndani ya mikoa hiyo bila kutegemea mazao kutoka maeneo mengine.

Waziri huyo ameitaka tume hiyo kusimamia kwa umakini miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha iliyowekezwa inaonekana na wakulima wanapata uzalishaji unaoendana na viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema Serikali imewekeza na inaendelea kuwekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wa Lindi na Mtwara wananufaika na miradi ya umwagiliaji hatua ambayo itawawezesha kufanya kilimo cha uhakika bila kutegemea mvua.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telacky amewataka wananchi kushirikiana na Tume katika kulinda miundombinu na rasilimali zilizowekezwa na Serikali kwa kuwa wao ndio wanufaika wakuu wa mradi huo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi Macklera Mrutu kutoka Tume amesema kuna jumla ya miradi 26 ya umwagiliaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara yenye thamani ya Sh23.7 bilioni hadi sasa miradi miwili iliyoanza na utekelezaji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na mifereji mirefu, mifereji ya kati ambapo itachukua hekta zaidi ya 300 na utekelezaji wake umefikia asilimia 27.