Aliyeua bibi yake kutokana na wendawazimu kuwa chini ya uangalizi

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imeamuru Hamis Fidel, aliyeshtakiwa kwa mauaji ya bibi yake, Selekwa Nditeze, kupelekwa kwenye taasisi ya watu wenye changamoto ya afya ya akili kama mkosaji mwendawazimu.

Hukumu hiyo imetolewa jana, Desemba 12, 2025, na Jaji John Nkwabi, aliyesema kutokana na mshtakiwa kuwa na changamoto ya afya ya akili, hana hatia ya mauaji.

Hata hivyo, ametoa amri kuwa awe chini ya uangalizi wa taasisi ya watu wenye tatizo la afya ya akili chini ya kifungu cha 235(3)(a) cha CPA.

Mauaji hayo yalitokea usiku wa Desemba 6, 2023, katika Kitongoji cha Munzeze, Kijiji cha Kishanga, wilayani Kasulu. Ilielezwa kuwa watu wawili, akiwemo Selekwa (marehemu), walijeruhiwa kwa panga.

Fidel Mayani, baba wa mshtakiwa, alijeruhiwa katika tukio hilo kwa kukatwa vidole vya mikono.

Hamis alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume cha Kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Shahidi wa nne, Fidel, alidai mahakamani kuwa siku ya tukio, walipomaliza kula chakula cha jioni, mke wake wa pili alikuwa amemuandalia maji ya kuoga, ghafla mshtakiwa alitokea na kumjeruhi kwa panga sehemu mbalimbali na kupoteza fahamu.

 Alidai alipokuwa hospitali akipatiwa matibabu, alijulishwa kuwa mama yake amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mshtakiwa.

Shahidi alidai mshtakiwa ni mtoto wake wa kiume wa mke wake wa tatu (Merciana).

Alieleza kuwa alibaini mshtakiwa ana tatizo la afya ya akili na walijaribu kumtibu kwa mganga wa kienyeji na hospitali bila mafanikio na kuwa kutokana na hali hiyo, mshtakiwa asingemuomba bibi yake tendo la ngono.

Alidai pia kuwa mshtakiwa aliwahi kumshambulia bibi yake (marehemu).

Shahidi wa tano, ambaye ni mke wa pili wa Fidel, alidai kuwa baada ya kushuhudia tukio hilo aliomba msaada kwa majirani. Alidai aliona mwili wa mama mkwe wake ukitolewa ndani, lakini hakuona aliyemuua.

Shahidi wa kwanza, Jeradi Fidel, aliieleza mahakama kuwa alimsaidia baba yake kumpeleka kituo cha afya.

Kuhusu afya ya akili ya mshtakiwa, alidai haikuwa sawa. Licha ya kutoshuhudia akiendesha kosa, alidai mazingira yalimfanya aamini kuwa mshtakiwa ndiye alihusika na mauaji hayo.

Shahidi wa sita alidai kuwa alijulishwa kuhusu mtu aliyekuwa juu ya mti akiwa na kamba kwa nia ya kujinyonga.

Baada ya kufika eneo hilo, walimshusha na kumpeleka kituo cha polisi ambako mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo.

Shahidi wa nane aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu aliieleza mahakama kuwa aligundua mwili ukiwa na majeraha ya kukatwa shingoni, kichwani, na kuchomwa na kitu chenye ncha kali. Alieleza kuwa chanzo cha kifo chake ni kupoteza damu nyingi.

Shahidi wa tisa, aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa, alidai kuwa mshtakiwa alimwambia kuwa alimuua bibi yake kwa sababu alikuwa akimuita jina baya.

Mshtakiwa alitegemea utetezi wa hali yake ya changamoto ya afya ya akili.

Shahidi wa kwanza wa utetezi, Dk Enock Changarawe, anayehudumia watu wenye matatizo ya afya ya akili, alieleza mahakama namna alivyomweka mshtakiwa kwa muda wa siku 14 chini ya uangalizi, akitumia mbinu mbalimbali na kubaini kuwa alikuwa mgonjwa wa akili wakati anatenda kosa.

Mshtakiwa akijitetea mahakamani alidai anakumbuka siku ya tukio alikuwa kijijini na kwamba bibi yake alifariki kwa kuwa alikuwa mgonjwa.

Alieleza alilalamika wajukuu wake hawakumtunza na hakumbuki kitu kingine. Baadaye alieleza alimkata bibi yake kwa panga, lakini hakutoka damu.

Jaji katika uamuzio wake aliangalia iwapo marehemu alifariki kwa kifo kisicho cha kawaida, iwapo mshtakiwa alimuua, iwapo mshtakiwa alikuwa na nia mbaya kabla ya kutenda kosa, na ikiwa shtaka limethibitishwa bila shaka yoyote.

Jaji Nkwabi amesema kuwa baada ya mahakama kuchambua ushahidi wa pande zote mbili, ikiwemo ushahidi wa Dk Changarawe, alithibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na tatizo la wendawazimu na alijikuta akifanya kosa hilo bila kujua athari zake.

Amesema mahakama inathibitisha kuwa ingawa mshtakiwa alikiri kumshambulia marehemu, alifanya hivyo akiwa na hali ya akili isiyo ya kawaida.

“Nathibitisha kwa uthabiti kwamba mshtakiwa alikuwa mwendawazimu wakati wa kutenda kosa hilo hata wakati wa utetezi wake. Hii ni kwa sababu utetezi wa tatizo la wendawazimu unapaswa kuthibitishwa kwa mizani ya uwezekano na bila shaka yoyote.

“Kuhusu iwapo kesi ya upande wa mashtaka imethibitishwa pasipo shaka yoyote, suala hili linajibiwa kuwa imeweza kuthibitisha kesi yake kwa kiwango nilichoeleza.”

Amesema kuwa ni uamuzi wa mahakama chini ya kifungu cha 235(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwamba mshtakiwa ana hatia lakini mwendawazimu, kwa sababu ya wendawazimu wake, hana hatia ya mauaji.

Ametoa amri kuwa mshtakiwa Hamis Fidel awekwe katika taasisi ya watu wenye tatizo la afya ya akili kama mkosaji mwendawazimu. Pia ameagiza nakala iliyoidhinishwa ya mchakato huo iwasilishwe kwa waziri husika.