KLABU nane zitashiriki Kombe la Mapinduzi 2026, baada ya msimu uliopita mashindano hayo kushirikisha timu za taifa na Zanzibar Heroes kuwa bingwa ilipoichapa Burkina Faso mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Desemba 28, 2025 na kumaliza Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, bingwa atakabidhiwa Sh150 milioni, ikiwa ni ongezeko la Sh50 milioni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Machano Makame Haji, amesema kwa upande wa Zanzibar timu tatu zitakazoshiriki ni Mlandege ambayo ni bingwa wa mwaka 2023 na 2024, Fufuni na KVZ. Kutoka Tanzania Bara ni Azam, Simba, Singida Black Stars na Yanga, pia kutakuwa na URA ya Uganda.
Naye, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe, amesema mshindi wa kwanza atavuna Sh150 milioni na wa pili Sh100 milioni. Kumbuka awali mshindi wa kwanza alipewa Sh100 milioni na wapili Sh70 milioni.
Pia, Waziri Pembe amesema kamati ya mashindano hayo itaundwa na watu 12 itakayoongozwa na Mwenyekiti, Machano, Makamu Mwenyekiti Mbarouk Suleiman Othman, Katibu ni Rashid Said Suleiman na wajumbe Khalid Bakari, Said Kasim Marine, Ramadhan Bukini, Hassan Mussa, Salum Ubwa, Hussein Abadalla Vuai, Mfamau Lali Mfamau, Ameir Makame na Kamal Abdulsatar Haji.
Mashindano hayo yalipoanza kufanyika mwaka 2007 katika mfumo wa sasa ukihusisha timu za Zanzibar na nje ya visiwani humo, Yanga ilikuwa ya kwanza kutwaa ubingwa, ikarudia tena mwaka 2021, msimu huu ina nafasi ya kutanua wigo wake wa ubingwa kufukuzia rekodi ya Simba iliyobeba mara nne (2008, 2011, 2015 na 2022) na Azam ikiongoza kwa kuchukua mara tano (2012, 2013, 2017, 2018 na 2019).
Timu zingine zilizofanikiwa kubeba ubingwa wa mashindano hayo ni Mlandege (2023-2024), Mtibwa Sugar (2010 na 2020), Miembeni (2009), KCCA (2014), URA (2016) na Zanzibar Heroes (2025).
Mashindano hayo yanafanyika kila mwaka, yakianzishwa kwa ajili ya kuadhimisha Mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar Januari 12, 1964.