Bodaboda watano waliokufa kwa kugongwa na lori watambuliwa

Dodoma. Miili yote mitano ya madereva wa bodaboda waliofariki dunia kwa ajali ya kugongwa na lori lililofeli breki eneo la Dodoma Makulu na kuwaparamia wakiwa kijiweni imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu.

Ajali hiyo ilitokea saa 2:30 usiku wa Desemba 11, 2025 wakiwa kwenye kijiwe chao cha Amani, wakisubiri wateja.

‎Waliofariki wametambuliwa kuwa ni Ishadi Jaa (25), Hafidhi Selemani (30), Adam Juma (27), Ijumaa Ndafu (27) na Michael Mkande (26).

‎Ndafu alizikwa jana Desemba 12 kwenye makaburi yaliyopo Dodoma Makulu, huku mwili wa Ishadi Jaa ukisafirishwa kwa maziko mkoani Arusha.

‎Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 13, Renatha Mzanje, Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, amesema marehemu wote watano waliopokewa hospitalini hapo wametambuliwa na miili yao imechukuliwa na jamaa zao.

‎‎”Miili yote mitano imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi, suala la wanazikwa wapi hatujui maana hiyo ni mipango ya familia tunaweza kusema wanazikwa Dodoma lakini wanafamilia wakaamua kusafirisha,” amesema.

Wakati huohuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema dereva aliyesababisha ajali hiyo bado anaendelea kutafutwa. Baada ya ajali dereva huyo alikimbia.

Akizungumzia ajali hiyo jana Desemba 12, Kamanda Hyera alisema mbali ya watu watano waliofariki dunia, utingo wa lori lililosababisha ajali alijeruhiwa ambaye Mzanje alieleza alikuwa akiendelea vizuri na matibabu.

Alisema athari nyingine iliyotokana na ajali hiyo ni uharibifu wa pikipiki na uzio wa nyumba iliyo jirani na barabara ambao uligongwa na lori hilo.

“Eneo hilo la barabara lina mteremko mkali, hivyo madereva ni lazima waendeshe mwendo wa tahadhari ili inapotokea changamoto yoyote waweze kuepusha maafa yanayoweza kuzuilika, tofauti na wanavyokuwa kwenye mwendo mkali,” amesema.

Hyera alisema kutokana na eneo hilo kuwa la hatari kwa waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu, Jeshi la Polisi litaimarisha usalama, wakati mamlaka nyingine ikiwamo Tanroads zikifanya jitihada za kuepusha ajali.