Bunge lataja sababu za kifo cha Jenista Mhagama

Dar es Salaam. Maradhi ya moyo umetajwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha aliyekuwa mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Bunge, Baraka Leornad leo Jumamosi Desemba 13, 2025 wakati akisoma wasifu wa marehemu Jenista, baada ya ibada ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

“Jenista Mhagama alifariki dunia Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma kwa maradhi ya moyo,” amesema Leonard.

Marehemu Jenista atazikwa Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.

Jenista Mhagama, alikuwa Mbunge wa Peramiho, aliyejijengea sifa kubwa kwenye siasa za Tanzania kupitia safari yake ya kiserikali iliyojaa vyeo vyenye umuhimu wa kitaifa na kikanda.

2000 – Mbunge wa Viti Maalumu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza.

2005 – Mhagama alichaguliwa kuwa Mbunge wa Peramiho kuwakilishwa wananchi wake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa miaka mingi, amekuwa mstari wa mbele katika kuwakilisha masilahi ya wafuasi wake na maendeleo ya jimbo lake.

2014 – 2015 – Baada ya kuonyesha ubora katika siasa za Bunge, Mhagama aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wadhifa uliompa nafasi ya kushirikiana na wizara katika kuboresha elimu ya ufundi nchini.

2015 – 2020 – Katika Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli (hayati), Mhagama aliteuliwa kuwa Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu. Hapa alishughulikia sera muhimu za ajira, masuala ya Bunge na masuala ya vijana na walemavu, akijitahidi kuboresha mfumo wa ajira na kushirikisha vijana katika maendeleo.

2020 – 2024 – Mhagama alihamishiwa katika Ofisi ya Rais kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais akilenga kuongeza uwajibikaji na uwazi wa Serikali kwa wananchi. Katika kipindi hiki, alichangia katika kuboresha utendaji wa mashirika ya umma na kufanikisha sera za uwajibikaji wa Serikali.

Agosti 2024 – Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Waziri wa Afya, nafasi ambayo amejitahidi kuitumia kuboresha huduma za afya, kupunguza changamoto za uhaba wa madaktari na kuongeza upatikanaji wa dawa na huduma za afya kwa wananchi.

Juni 2025 – Kati ya mafanikio yake ya kikanda, Mhagama alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Afya (Regional Steering Committee – ResCo) Ukanda wa Mashariki mwa Afrika, nafasi inayomuwezesha kushirikiana na mawaziri wenzake wa Kiafrika katika kuboresha sekta ya afya kieneo.

Jenista Mhagama alijipatia sifa ya kuwa kiongozi wa karibu na wananchi wake, na ni mmoja wa wanasiasa wanawake wenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania. Safari yake inaonyesha ukuaji wa kiserikali kutoka mbunge wa jimbo hadi waziri wa afya mwenye jukumu la kikanda.