TAARIFA mbaya kwa klabu Yanga ni kwamba, kiungo wao wa zamani Chico Ushindi amefariki dunia leo Desemba 13, 2025 akiwa kwao DR Congo.
Mmoja wa maofisa wa klabu ya DON Bosco ambayo amewahi kuitumikia nyota huyo akitokea TP Mazembe, amethibitisha kwamba Chico amefariki baada ya kuugua kwa siku chache.
Bosi huyo amesema Chico, alikuwa sawa kiafya wiki iliyopita lakini mambo yalibadilika katikati ya wiki hii ambapo alipopelekwa hospitali Jumatano Desemba 10, 2025, hakuweza kurudi hadi umauti unamfika.
“Alikuwa sawa kabisa lakini ameugua siku kama tatu tu na leo tumeambiwa amefariki, viongozi walikwenda kumuona wakasema anaendelea vizuri,” amesema bosi huyo.
Chico aliitumikia Yanga kwa muda mfupi, usajili wake ulitangazwa Januari 16,2022 akitokea TP Mazembe. Hata hivyo, Chico hakudumu sana ndani ya Yanga akiichezea kwa miezi sita pekeee na kurudi kwao DR Congo.
Wakati Chico akitua Yanga, dili hilo lilimvusha aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mukoko Tomombe ambaye alielekea TP Mazembe.
