Dk Nchimbi: Wananchi wa Peramiho hawana malalamiko na Jenista

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika kipindi chote cha miaka 25 ambayo Jenista Mhagama amekuwa mbunge wa Peramiho, wananchi wake hawana malalamiko juu yake.

Amesema hali hiyo ilitokana na kazi kubwa aliyofanya, akitanguliza maslahi ya wananchi mbele na kuwatumikia kwa upendo.

Jenista amekuwa mbunge kwa miaka 25, naibu waziri kwa mwaka mmoja na waziri kwa miaka 10. Amefariki dunia Desemba 11, 2025, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.

Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo, Desemba 13, 2025 wakati akitoa salamu katika ibada ya kuaga mwili wa mbunge huyo, iliyofanyika katika Kanisa la Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

Amesema wananchi hawana malalamiko kwa sababu alikuwa mtumishi wa kweli kwa watu wake alikuwa mnyenyekevu na kupenda sana watu wake.

Katika kipindi chote cha utumishi wake, Jenista alitanguliza mbele kuwatumikia wananchi waliomchagua na hata alipokuwa waziri, hakuacha kuwahudumia wananchi, huku akiguswa zaidi na wanyonge.

“Ndiyo maana leo wanyonge wa Peramiho wana uchungu kuliko mtu yeyote, kwa sababu wanajua mpiganaji wao, mtetezi wao ameondoka na kutangulia mbele za haki. Ni ombi letu kuwa wapate mtumishi mwingine wa aina yake,” amesema.

Amesema wakati akitafakari kifo cha Jenista, aliwaza kuwa kama Mungu angemwambia aombe jambo moja, basi angeomba wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na madiwani wote wawapende na kuwatumikia watu wao kwa kiwango alichokuwa nacho Jenista.

“Tumeletwa duniani si kuishi tu bali kuwatumikia wenzetu. Ni utumishi kwa binadamu wenzetu unaotupa heshima mbele ya Mungu na kuwafanya watu watukumbuke kwa kazi tulizozifanya,” amesema.