Familia, Zungu walivyomuelezea Jenista Mhagama

Dar es Salaam. Mtoto wa marehemu, Victor Mhagama, amesema wakati wengine wakimuita Jenista Mhagama kiongozi, wao walimuita mama na katekista kwa sababu alikuwa mwalimu wa dini nyumbani.

“Tulimpenda sana mama, tuliishi naye kwa karibu na upendo naye aliunganisha sana familia yetu,” amesema Mhagama.

Ametoa kauli hiyo wakati akitoa neno la familia katika ibada ya kuaga mwili wa mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, uliofanyika katika Kanisa la Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, leo, Desemba 13, 2025.

Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, alifariki dunia Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Victor amesema mama yake alipougua kwa muda mfupi, walitoa taarifa kwa viongozi, na wanashukuru namna ambavyo Serikali iliwasadia kwa uharaka hadi kufika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambapo umauti ulimkuta.

Amesema mama yao alikuwa na sifa za kipekee, kwani kuna siku za sikukuu alikwenda kazini, alipoulizwa kwanini, alisema, “Asipojenga nchi nani atajenga?” na kutaka wamsaidie Rais kufanya kazi.

“Mama aliamini katika kuchapa kazi, alitusihi wote tupende nchi yetu, tuwe wazalendo, tuchape kazi hakuna namna nyingine. Alitusihi wote tuliopita kwenye mikono yake, uchaji wa Mungu, elimu pia kwa sababu alipenda kusoma, hivyo nyumbani vilijaa vitabu,” amesema.

Almeasihi Watanzania kuenzi maisha yake kwani marehemu alijali utu, fadhila, hakujali mkubwa wala mdogo, maskini wala tajiri, bali aliwasimamia kwa haki na upendo.

“Ushuhuda wa wengi waliojaa humu waliguswa na maisha ya mama na walimfahamu katika nafasi mbalimbali. Ninawaomba tuendelee kuishi katika ukristo wake na tukikumbuka kuwa aliipenda nchi na wana Peramiho,” amesema.

Amesema, kwa kushirikiana na Serikali, miradi mingi imekwenda Peramiho ikiwemo shule, zahanati, barabara, huku akisema mama yake hana deni na amewasitiri sana wana Peramiho.

“Hata mkifanya buriani, mkiangalia uso wake umejaa tabasamu kwa sababu njia aliyoipita ni salama, tuipite pia katika imani, ushirikiano na maendeleo, kwa sababu hakupenda kulala nyuma na alipenda kujifunza. Alitushajihisha kwa sababu alitaka matokeo muda wote,” amesema.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema Jenista alikuwa kiongozi aliyeipenda nchi yake na kazi zake.

Tangu Jenista aingie bungeni mwaka 2005, alimzoea akimuita Zungu mwanaye, na Zungu akimuita mama, huku akisema wameishi naye vizuri.

“Sifa zilizotolewa hapa na baba Paroko ni za ukweli, ni mtu aliyejishusha sana. Kikubwa, kumuombe Mungu ampokee, amchukue, amuweke pema yeye na wengine waliotangulia mbele za hakai,” amesema Zungu.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyokuwa na Bunge karibu wakati wa msiba, na hatua ya kutoa ndege kwa ajili ya kupeleka mwili kwenda kumpumzisha Songea.

“Niwaombe familia, msiba huu ni mtihani na ni mzito sana, shikamaneni, pendaneni, msisikilize maneno ya kuwagawa. Hakuna jambo ambalo Mungu analipenda kama umoja,” amesema.

Amesema familia hiyo ilipata bahati ya kuwa na mama mwema, huku akiwataka kuendeleza wema wake.