Dodoma. Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Padri Emmanuel Mtambo amesema mbali na utumishi wa Serikali na nyanja za kisiasa, marehemu Jenista Mhagama alikuwa ni mtumishi mwaminifu wa kanisa hilo.
Paroko Mtambo ametoa kauli hiyo wakati wa mahubiri yake kwenye ibada ya kuaga mwili wa Mhagama ndani ya kanisa hilo leo Jumamosi Desemba 13, 2025.
Paroko huyo amesema katika kipindi cha uhai wake, Mhagama alikuwa ni mfano wa utumishi na utoaji wa zaka ikiwemo misaada kwa wasiojiweza ambapo mara nyingi alikuwa akitoa sadaka lakini hakutaka atangazwe.
“Mara kadhaa alikuwa akimtuma dereva wake kuleta sadaka hiyo lakini alikataa kutangazwa hadharani na ndivyo tulivyofanya,” amesema Padri Mtambo.
Kiongozi huyo wa kiroho, ameeleza kuwa hata vazi alilolivaa leo wakati akiongoza ibada alikuwa amelipiwa na Mhagama, akaliagiza kutoka Kenya.
Kingine, amesema amewasaidia kanisani hapo kujenga minara na sanamu ikiwemo sanamu kubwa ya Bikira Maria ambayo imejengwa katika eneo la kuingia kanisani ambavyo alikuwa akifanya kwa hiyari yake bila kulazimishwa.
