Katibu wa Bunge Aeleza Chanzo cha Kifo cha Jenista Mhagama – Video

Chanzo cha kifo cha aliyekuwa Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, marehemu Jenista Joakim Mhagama, kimetajwa kuwa ni maradhi ya moyo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 13, 2025 na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, wakati akisoma wasifu wa marehemu katika misa takatifu ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Jenista Mhagama, iliyofanyika jijini Dodoma, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, marehemu alifariki dunia Desemba 11, 2025 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Jijini Dodoma.

Katika wasifu wake, marehemu Jenista Mhagama ametajwa kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa katika sekta ya afya, Bunge na maendeleo ya jamii, akitumikia Taifa kwa uadilifu na kujitolea hadi mwisho wa maisha yake.

Ibada hiyo ya kuaga imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wabunge, viongozi wa dini, wanafamilia, pamoja na waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi, huku Taifa likiendelea kuomboleza msiba huo mkubwa.