KAMA wewe ni shabiki na mpenzi wa Simba uliyekuwa ukitamani kusikia au kuona Kocha Seleman Matola anapigwa chini Msimbazi, basi pole yako, kwani sasa ni rasmi chuma hichi kimebaki.
Hii ni kwa sababu mabosi wa klabu hiyo wameamua kwa kauli moja kumbakisha mwamba huyo kama kocha msaidizi nafasi anayoishikilia tangu mwaka 2019 alipotua Msimbazi akitokea Polisi Tanzania, wakati wakimsikilizia kocha mkuu mpya anayetarajiwa kutangazwa muda wowote.
Siyo kumbakisha tu Msimbazi, lakini mabosi wa Simba wamejipanga kumtengenezea mazingira mazuri Matola kwenda kupata uzoefu zaidi nje ya nchi kabla ya kuja kukabidhiwa rasmi timu hiyo akiwa kocha mkuu rasmi, hii ni kutokana na kuthamini mchango wake tangu akiwa mchezaji hadi ukocha.
Ndiyo. Kama unakumbuka jana Mwanaspoti liliwadokezea kupitishwa rasmi kwa jina la kocha mkuu mpya ambaye hata hivyo bado imefanywa siri kubwa kwa jina lake, lakini kukiwa na mgawanyo kuhusu Matola kama asepeshwe jumla klabuni au aachiwe timu kutegemea na msimamo wake.
Sasa zikufikie taarifa, Matola bado yupo sana Msimbazi baada ya kikao cha vigogo wa klabu hiyo kilichofanyika Jumatano kuamua kwa kauli moja kumbakisha, japo wanasikilizia kile atakachokuja nacho kocha mkuu mpya wanayemalizana naye kabla ya kumtangaza hivi karibuni.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kililiambia Mwanaspoti, baada ya majadiliano mazito ya wajumbe wa kikao hicho kilichohusisha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba na vigogo wengine, Matola asalie kama kocha msaidizi na asipewe timu jumla kama kocha mkuu.
Hata hivyo, inadaiwa mabosi hao watamsikilizia kocha mkuu mpya ajaye kama ataamua kuja na benchi nzima basi Matola atarudi kusimamia timu za Wanawake na Vijana, kisha watampeleka nje ya nchi katika klabu mojawapo kati ya zile marafiki za Simba ikiwamo ya Ujerumani na nyingine Asia.
“Kama kocha atasema anataka kufanya naye kazi, atasalia kama kocha msaidizi kwa nafasi aliyonayo kwa muda mrefu, lakini akisema anataka aje na benchi lake jipya lote, hii itakuwa na maana, Matola atarudi katika cheo chake cha zamani cha kusimamia timu za Vijana na Wanawake,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mmoja wa vigogo wa Simba.
“Akiwa na timu za vijana na wanawake, Matola atapelekwa nje ya nchi kuongeza ujuzi zaidi kwa muda wa miezi sita kati ya klabu moja huko Ujerumani au Asia ambapo atafundisha na kusoma, kisha atakaporejea aje kuwa kocha mkuu rasmi wa Simba,” kiliongeza chanzo hicho na kusisitiza;
“Hii imetokana na ukweli, Matola ni kijana wetu, amechezea kwa ufanisi akiwa nahodha na kwa muda mrefu amekuwa kocha aliyesomeshwa na klabu, ni ngumu kumtema moja kwa moja, ikizingatiwa pia ana mkataba hadi mwisho mwa msimu.
Awali inadaiwa, Matola mwenyewe alipigiwa simu na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo wakati wa kikao hicho na kumuuliza juu ya mipango yake na mwenyewe amesema alikuwa anataka kusepa ili akapate changamoto nyingine mpya nje ya Simba.
“Jibu hilo ni kama liliwavuruga wajumbe na kumtaka atulie wajadili kisha watamrudia na kweli baadae sana baada ya maamuzi ya pamoja, walimwambia hawakubaliani na msimamo wake wa kuondoka kwa vile wanajua hana tatizo na kufanya vibaya kwa timu kunachangiwa na mengi.”
“Hata hivyo, jibu hilo halikukubaliwa kirahisi na Matola, aliyesema kuondoka kwake kunaweza kuepusha mengi, kwa vile mashabiki na wapenzi wa Simba wamekosa imani naye baada ya kupoteza mechi ya Azam na hataki kuona timu ikiyumba kwa sabababu yake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Matola amesema anaamini kwa uwezo na ujuzi alionao anaweza kufanya kazi kokote na kuonyesha kipaji alichonacho kama alivyofanya enzi akiwa na Lipuli kabla ya Polisi Tanzania kumchukua kwa muda mchache na baadae Simba kuamua kumrudisha ilipomtema Patrick Aussems.”
Chanzo hicho kinasema baada ya majadiliano ya kina na kuelezwa mipango aliyowekewa na mabosi hao hao ikiwamo kupelekwa Ulaya au Asia kuongeza ujuzi kupitia klabu rafiki, Matola alilegeza msimamo.
“Japo kubaki kama kocha msaidizi au kwenda timu za vijana na wanawake itategemea kitakachoamuliwa na kocha mkuu ajaye, ila Matola hatoki Msimbazi leo ama kesho, kwani Simba bado ina malengo makubwa naye kama heshima ya alichokifanya kwa miaka mingi kwa Simba,” kilisisistiza chanzo hicho.
Matola alikaimishwa timu mara baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, japo alitambulishwa kama meneja mkuu, Dimitar Pantev kusitishiwa mkataba mara Simba ilipopoteza mechi ya pili mfululizo ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Stade Malien ya Mali.
Awali Simba ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Petro Atletico du Luanda ya Angola, ndipo mabosi walipomalizana na Pantev kwa makubaliano ya pande mbili na Matola kuachiwa kuiongoza katika mechi mbili za Ligi Kuu akipata ushindi wa 3-0 dhidi ya Mbeya City kabla ya kulala 2-0 kwa Azam FC na kuibukia kelele kwa wanasimba wakitaka aondolewe kabla ya kikao hicho.
Mashabiki na wapenzi wa Simba walitaka Matola aondolewe kwa madai kama makocha wakuu wakizingua wanaondolewa iweje yeye abakishwe mara zote, kitu kinachodaiwa kimechochea hata yeye kutaka kuondoka jumla kabla ya mabosi wa klabu hiyo kumgomea kwa heshima aliyonayo kwao.
Katika miaka sita ya Matola akiwa kocha msaidizi Simba, amefanya kazi na chini ya makocha 10 tofauti, wakiwamo tisa wa kigeni tisa na mmoja mzawa, timu ikitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la FA na timu hiyo kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopoteza kwa RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba inatarajiwa kurejea tena uwanjani mapema mwakani kwa mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance iliyopo nafasi ya tatu kundini na pointi mbili na malengo ya klabu ni kutaka kocha mkuu mpya atue mapema aiandae timu sambamba kusajili dirisha dogo.
