Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo
ameongoza familia, viongozi, wabunge na waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama, iliyofanyika
katika Kanisa la Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege,
Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Rais Dkt. Samia alieleza masikitiko makubwa ya Taifa kufuatia msiba huo, akimwelezea
marehemu kuwa alikuwa kiongozi jasiri, mwaminifu na mlezi wa viongozi wengi ndani
ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyelitumikia Taifa kwa moyo
wa kujitoa, nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu, akisimama imara kutetea haki,
maendeleo na usawa wa wananchi.
Aidha, alitambua mchango mkubwa wa Marehemu akihudumu kwa ufanisi katika nafasi
mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi, sambamba na uwezo
wake wa kubeba majukumu mazito kwa weledi.
Akigusia urithi wa uongozi aliouacha, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa moyo wake wa
kujali maslahi ya Taifa ndio nguzo kuu ya kumbukumbu ya Hayati Jenista Mhagama, na
kutoa wito kwa wabunge na viongozi wote kuiga mfano wake wa maadili na uwajibikaji
aliouonesha.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi kuuenzi mchango wa Marehemu kwa
kuimarisha misingi ya uwajibikaji, mshikamano wa kitaifa na utumishi unaolenga maslahi
mapana ya wananchi.
Rais Dkt. Samia alitoa pole kwa familia, ndugu, wananchi wa Jimbo Peramiho, Bunge na
Taifa kwa ujumla, na kumuomba Mwenyezi Mungu awape faraja, nguvu na amani, huku
akiiombea roho ya Marehemu pumziko la amani ya milele.