Masauni achaguliwa Makamu wa Rais UNEA

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni amechaguliwa kuwa makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA).

Masauni amechaguliwa kushika nafasi hiyo katika mkutano wa saba wa baraza hilo, uliofanyika kwa muda wa wiki moja jijini Nairobi, Kenya.

Mbali na Masauni, baraza hilo pia limemchagua Matthew Samuda kuwa Rais wa baraza hilo ambalo limekamilisha mkutano wake wa saba na kutoa maazimio 11 yanayolenga kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayoanuwai, uharibifu wa ardhi, uchafuzi wa mazingira na taka.

Baada ya uongozi huo kutangazwa, Rais Samuda amesema uongozi wake utakwenda kupaza sauti zitakazokuwa mstari wa mbele kwenye jamii katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Kama Rais, naahidi kukuza Bunge lenye ujumuishi, uwazi na hatua za vitendo, kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha muunganisho wa sayansi na sera, kuongeza ufadhili wa kukabiliana na hali na ustahimilivu na kuharakisha mpito hadi mifumo endelevu ya uzalishaji na matumizi,” amesema Samuda.

Ameongeza kuwa chini ya uongozi wake, baraza hilo litajikita kufanya kazi katika misingi ya usawa na kuhakikisha kuwa hakuna jambo kubwa au dogo linalotengwa katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Mkutano huo, pia, ulipitisha maazimio kadhaa kwa nchi wanachama kuhusu uhifadhi wa mazingira ikiwemo kulinda miamba ya matumbawe, usimamizi mzuri wa madini na metali, usimamizi mzuri wa kemikali na taka na matumzi ya akili bandia katika kutafuta suluhisho endelevu kupitia michezo.

Mengine yaliyopitishwa yalilenga ushirikiano wa kimataifa ili kupambana na moto wa nyikani, kuimarisha kazi kuhusu kipimo cha mazingira cha upinzani dhidi ya vijidudu, kulinda barafu na kushughulikia maua ya mwani wa sargassum na mengineyo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya watu 6,000 wanaowakilisha nchi 186 ambao waliojiandikisha kushiriki mkutano wa wiki nzima, uliofanyika katika makao makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi.