Maswa. Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) imetangaza kuanza kwa mgawo wa maji katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, kutoka na upungufu wa maji katika vyanzo vyake vya maji, likiwemo bwawa la New Sola, ambalo ndiyo chanzo kikuu cha maji.
Akizungumza leo Desemba 13, 2025, na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias, amesema hali hiyo imesababishwa na ukame unaoendelea pamoja na kuchelewa kwa msimu wa mvua, hali iliyosababisha kushuka kwa kiwango cha maji katika vyanzo vya uzalishaji.
Amesema, kutokana na hali hiyo, mamlaka imelazimika kuanza rasmi mgawo wa huduma ya maji kuanzia Desemba 20, 2025, katika maeneo yote ya Wilaya ya Maswa, ili kuhakikisha maji yanayopatikana yanatumika kwa usawa.
“Kwa sasa, uzalishaji wa maji umepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na vyanzo vyetu kuwa na maji machache. Ili kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa usawa kwa wakazi wote wa Maswa, tumeona ni lazima kuanzisha mgao wa maji kuanzia Desemba 20, 2025,” amesema.
Ameeleza kuwa mgawo huo utafanyika kwa ratiba maalumu itakayowasilishwa kwa wananchi kupitia viongozi wa mitaa, vitongoji, na vijiji, pamoja na matangazo ya umma, huku akitoa wito kwa wananchi kutumia maji kwa uangalifu mkubwa pamoja na kutoa taarifa mapema kuhusu uvujaji wa maji pindi unapobainika katika maeneo yao.
“Tunawasihi wananchi kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya maji na kushirikiana nasi katika kipindi hiki kigumu tunaposubiri kurejea kwa mvua za msimu. Wakati wananchi wanapobaini uvujaji wowote wa maji, watupatie taarifa mapema,” amesema.
Ameongeza kuwa Mauwasa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha huduma ya maji inarejea katika hali ya kawaida mara hali ya vyanzo itakapokuwa imetengemaa.
Esther Festo, mkazi wa Majebele mjini Maswa, amesema mgawo wa maji utawalazimu kubadili mwenendo wa matumizi ya maji majumbani.
“Itakuwa changamoto kidogo, hasa kwa familia zenye watoto, lakini hatuna budi kutumia maji kwa uangalifu ili yatuvushe kipindi hiki cha muda mfupi,” amesema.
Kwa upande wake, Juma Ally, mkazi wa mtaa wa Ziota mjini Maswa, ameipongeza Mauwasa kwa kutoa taarifa mapema.
“Ni jambo jema, wametutangazia mapema. Hii itatusaidia kuhifadhi maji na kupanga matumizi yetu vizuri,” amesema.
Naye Juma Hassan, mfanyabiashara wa chakula, amesema mgawo wa maji unaweza kuathiri biashara ndogo ndogo.
“Biashara kama zetu zinategemea sana maji. Bila mpangilio mzuri wa mgao wa maji, shughuli nyingi zinaweza kusimama,” amesema.