Mavunde ataka kasi ukamilishaji miradi ya kimkakati sekta ya madini

Dar es Salaam. Serikali imeendelea kuipa sekta ya madini nafasi ya kimkakati katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, ikilenga kuibadilisha kutoka sekta ya uchimbaji wa madini ghafi kwenda sekta ya thamani, viwanda na ajira.

Mwelekeo huo unaonekana kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mafunzo, uimarishaji wa wachimbaji wadogo, usimamizi wa masoko ya madini, na utekelezaji wa mikataba ya madini ya kimkakati.

Hatua mojawapo ya utekelezaji wa mkakati huo ni ujenzi wa jengo la kituo cha mafunzo ya uongezaji thamani madini ya vito nchini, cha Kituo cha Gemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha.

Akikagua mradi huo jana, Desemba 12, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesisitiza umuhimu wa kasi na ubora katika utekelezaji wa mradi huo.

“Serikali inahitaji ujenzi bora unaokidhi vigezo vyote vilivyoainishwa kwenye mkataba. Mkandarasi aongeze nguvu kazi na kufanya kazi kwa saa 24 ili mradi huu ukamilike kwa wakati, kwa kuwa ni mradi wa kimkakati kwa taifa,” amesema.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009, inayolenga uongezaji thamani katika mnyororo mzima wa madini, akisisitiza kuwa Serikali imeamua kutekeleza sera hiyo kwa vitendo.

“Serikali imedhamiria kuona madini ya vito yanaongezewa thamani hapa nchini, hatuwezi kuendelea kusafirisha madini ghafi wakati tuna uwezo wa kujenga wataalamu, viwanda na ajira ndani ya nchi,” amesema.

Aidha, Mavunde amefafanua kuwa kuanza kwa ujenzi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa hotuba yake ya kulihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu na miundombinu ya sekta ya madini.

Kwa mujibu wa Mavunde, kukamilika kwa kituo hicho kutachochea ongezeko la wanafunzi, wataalamu wa uongezaji thamani madini ya vito, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wafanyabiashara wa madini, pamoja na kupunguza usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na hivyo kuongeza mapato ya taifa.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa akizungumza na watendaji alipokagua shughuli za uchimbaji wa madinji katika ziara yake Same, Mkoani Kilimanjaro jana, Ijumaa Desemba 12, 2025.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amethibitisha kuwa Serikali wilayani humo itaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, ili kuzingatia maelekezo ya Serikali.

“Tutahakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati kama Serikali inavyotaka, kwa kuwa ni uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya madini mkoani Arusha na taifa kwa ujumla,” amesema.

Akitaja gharama za ujenzi huo, Mkuu wa Kituo cha Gemolojia (TGC), Mhandisi Ally Maganga, amesema mradi huo wa majengo pacha ya ghorofa nane utagharimu Sh33 bilioni na utaongeza uwezo wa taifa katika mafunzo ya uongezaji thamani madini ya vito.

“Kukamilika kwa majengo haya kutapanua wigo wa mafunzo, kuongeza idadi ya wanafunzi na kuchochea ajira kwa vijana kupitia ujuzi wa gemolojia na uongezaji thamani wa madini ya vito,” amesisitiza.

Sambamba na uwekezaji katika miundombinu, Serikali inaendelea pia kushughulikia changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo na wadau wa madini nchini.

Kauli hiyo imethibitishwa na Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, aliyoitoa jana, Desemba 12, 2025, akiwa ziarani wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, alipokagua shughuli za uchimbaji wa madini.

“Serikali inatarajia kukutana na wadau wa madini ya jasi jijini Dodoma ili kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto zinazoathiri biashara ya madini hayo,” ameahidi.

Dk Kiruswa pia amekemea vitendo vya kununua na kuuza madini ya jasi chini ya bei elekezi iliyotolewa na Tume ya Madini, ili kulinda thamani na tija ya madini hayo nchini.

“Bei elekezi ipo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wachimbaji, hakuna mtu atakayevunja miongozo ya Serikali na kuendelea kuwaumiza wananchi,” amesisitiza.

Ili kuhakikisha sekta ya madini inaendelea bila kuathiri mazingira, Dk Kiruswa amewataka wachimbaji kuhakikisha wanafukia mashimo mara baada ya kukamilisha shughuli za uchimbaji.

“Utunzaji wa mazingira si hiari bali ni wajibu kwa kila mchimbaji anayefanya kazi chini ya leseni ya Serikali,” amesisitiza.

Aidha, ametilia mkazo umuhimu wa mafunzo ya uongezaji thamani madini (MBT), utoaji wa leseni na matumizi ya vifaa vya kisasa ili kuongeza tija, usalama na ushiriki wa vijana na wanawake katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Akizungumza alipozindua Bunge jijini Dodoma, Rais Samia alitoa mwelekeo wa Serikali awamu ya sita katika muhula wake wa pili kwenye sekta ya madini, akiitaja sekta hiyo kuwa chocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi.

“Sekta ya madini ina nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya sekta nyingine, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuinua pato la Taifa,” alisema.

Rais Samia pia alisisitiza kuwa kufuatia matamko ya mataifa ya nje kusitisha misaada kwa Tanzania, Serikali inapaswa kuboresha matumizi ya rasilimali za ndani ili kumudu mahitaji ya nchi bila misaada.

Mbali na maelekezo hayo, katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya madini imeainishwa kama eneo la kimkakati litakalowezesha Tanzania kuongeza mapato ya ndani, kukuza viwanda na teknolojia.