Raia wa Ghana Frederick Kumi maarufu mtandoni ‘Abu Trica’ amekamatwa kwa tuhuma za utapeli wa kimapenzi na kuwaibia wazee na watu wazima ambao ni Wazungu nchini Marekani kiasi cha fedha Dola milioni 8 za Marekani.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema kijana huyo mwenye miaka 31, alitumia zana za akili bandia (AI) kuunda utambulisho usio wa kweli, pia aliwasiliana na waathiriwa kupitia tovuti za kutafuta wapenzi na mitandao ya kijamii, kisha polepole akajenga imani yao kabla ya kuwaomba fedha.
Abu Trica anakabiliwa na mashtaka nchini Marekani ya kula njama ya kufanya udanganyifu wa kielektroniki (wire fraud) na utakatishaji wa fedha na akipatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela.
Wachunguzi wanasema Abu Trica, ambaye pia hutumia jina jingine Emmanuel Kojo Baah Obeng, amekuwa akiwasiliana na kina mama hao watu wazima kupitia simu, baruapepe na ujumbe wa maandishi.
Inadaiwa mbinu ambayo hutumia kuwapata huanza kwa kuwaeleza taarifa za kusikitisha zinazomhusu za kiafya, matatizo ya safari au fursa za biashara akiwa na lengo kuwashawishi kutuma fedha au vitu vya thamani.
Waendesha mashtaka wanasema fedha hizo zilimfikia kupitia aliowaita watu wake wa karibu, huku akidaiwa kuzitumia na washirika wake walioko Ghana na Marekani.
Inaelezwa kuwa kijana huyo mwenye wafuasi zaidi ya 100,000 kwenye Instagram, mara kwa mara amekuwa akionyesha mavazi ya kifahari, vifaa vya kisasa na vito, hali iliyozua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo.
Mtandao wa African News umechapita taarifa hiyo jana Desemba 12, 2025, ikieleza kuwa kijana huyo amekamatwa nchini Ghana baada ya operesheni ya pamoja kati ya mamlaka za Marekani na Ghana.
Marekani sasa inatafuta kumrudisha nchini humo (extradition) chini ya sheria zinazolenga kulinda Wamarekani wazee dhidi ya unyanyasaji wa kifedha.
Kesi yake ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa hatua zinazochukuliwa na mamlaka za Marekani dhidi ya mitandao ya ulaghai inayodaiwa kufanya kazi kutoka Afrika Magharibi. Mwezi Julai, mwanaume mwingine kutoka Ghana anayejulikana mtandaoni kama Dada Joe Remix alihamishwa kwenda Marekani kwa tuhuma za utapeli kama huo.
Mapema mwezi huu, kinara wa ulaghai kutoka Nigeria, Oluwaseun Adekoya, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kutakatisha zaidi ya dola milioni 2 zilizohusishwa na utapeli wa benki na mtandaoni kote nchini.
Maofisa wa Marekani wanasema wanaongeza shinikizo kwa makundi ya kihalifu yanayowalenga Wamarekani wazee kupitia mipango ya kimapenzi na kifedha ya ulaghai.
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa Mashirika.
