Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amesema hayo wakati wa hafla ya kuhitimisha mbio za Utumishi Marathoni 2025 zilizoandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Mtwara.
Akiwasilisha salamu za Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mwaipaya amesema, “Historia ya Chuo cha Utumishi wa Umma ni sehemu muhimu ya mafanikio ya utumishi wa umma nchini. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, chuo hiki kimekuwa mhimili muhimu wa kutoa elimu, mafunzo, na ujuzi unaowawezesha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, na ufanisi.”
Pia, Mhe. Mwaipaya amepongeza Chuo kwa maandalizi mazuri ya tukio hili na kusema kuwa mbio za marathoni si tu zinaboresha afya na mshikamano, bali pia zinaunda hisia za uzalendo na utu miongoni mwa washiriki. Ameongeza kuwa, “Marathon hii si tukio la michezo tu; ni kumbukumbu hai ya safari ndefu na mafanikio makubwa ambayo chuo chetu kimeipitia kwa kipindi cha miaka 25. Amessitiza kuwa, safari ya miaka ishirini na tano imejengwa juu ya misingi ya nidhamu, ubunifu, ushirikiano, na kujituma kwa manufaa ya taifa letu.”
Naye Makamu Mkuu wa Chuo -Taaluma, Tafiti na Shauri za Kitaalam, Dkt. Hamisi Amani, aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo na kuwa Mtendaji Mkuu, amesema kuwa safari ya miaka 25 ya chuo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ni jambo la kujivunia.
“Leo si tu tunakimbia kwa ajili ya afya na umoja, bali tunasherehekea mafanikio, historia, na mchango mkubwa wa chuo kwa taifa letu kwa takribani robo karne,” amesema Dkt. Amani.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Chuo kimepata maendeo makubwa na mabadiliko chanya katika utoaji wa elimu, uboreshaji wa huduma, na katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa umma nchini.
Dkt. Amani amesema kuwa, mafanikio yaliyopatikana nia ni pamoja na kupanuka kwa kampasi kutoka mbili hadi sita, kuongezeka kwa kozi na programu za muda mrefu, kuboreshwa kwa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa umma na matumizi yaa teknolojia katika kutoa mafunzo jambo liliwezesha chuo kuwafikia watumishi wa umma wengi kwa urahisi.
Akihitimisha hotoba yake, Dkt. Amani amesema kuwa, Utumishi Marathon 2025 ni sehemu ya maadhimisho yanayofanyika kwa kampasi zote za chuo cha utumishi wa umma Tanzania na kusema kuwa kilele cha maadhimisho haya kifanyika mapema mwakani.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya akiongea na washiriki wa Mbio za Marathon 2025 katika kuadhimisha Miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika tarehe 13 Desemba 2025 katika Kampasi ya Mtwara
Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti za Kitaalamu, Dkt. Hamisi Amani akizungumza wakati wa Utumishi Maraton 2025
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akiwa na Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti za Kitaalamu, Dkt. Hamisi Amani, wakiwa tayari kuanzisha Utumishi Marathon 2025 katika viwanja vya Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Mtwara. Mbio hizi ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania leo tarehe 13 Desemba 2025 Manispaa ya Mtwara.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
