LICHA ya beki wa kati wa Fountain Gate, Mrundi Derrick Mukombozi kubakisha mkataba wa miezi sita na kikosi hicho, ila timu mbalimbali zimeanza kuiwinda saini yake dirisha dogo la Januari 2026, zikiwemo za Pamba Jiji na TRA United.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo, ameiambia Mwanaspoti ni kweli nyota huyo anafuatiliwa na timu mbalimbali dirisha dogo la Januari 2026, huku Pamba na TRA United zikiwa mstari wa mbele kumhitaji, japo hakuna muafaka wowote uliofikiwa.
“Hasa sasa timu hizo mbili ndizo zimeonyesha uhitaji kwake japo kama nilivyosema mwanzoni hakuna muafaka uliofikiwa kwa sababu mchezaji mwenyewe ana mkataba bado wa miezi sita uliobakia, hivyo, acha tuone itavyokuwa,” kimesema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mukombozi amesema bado ni mchezaji halali wa Fountain Gate kwa sababu ana mkataba, japo kama kutakuwa na jambo lolote kipindi hiki linalohusu mustakabali wake katika kikosi hicho, mashabiki zake watajua mapema.
“Unapofikia wakati huu wa usajili kila mtu anazungumza lake, suala la kuondoka kwa sasa siwezi kulizungumzia kwa sababu bado ni mapema na lolote linawezekana, mashabiki zangu watambue nipo Fountain na nina mkataba nao,” amesema Mukombozi.
Nyota huyo alijiunga na Fountain Gate akitokea Namungo aliyoitumikia kwa mkataba wa miezi sita tangu alipoondoka msimu wa 2023-2024 na alijiunga na ‘Wauaji wa Kusini’ kwa mara ya kwanza Agosti 24, 2023, akitokea Nkana FC ya Zambia.
Kwa msimu wa 2023-2024, beki huyo alifunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu wa 2024-2025, alitupia moja tu katika ushindi wa Namungo wa 2-1, dhidi ya Mashujaa, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi, Aprili 20, 2025.
Beki huyo licha ya kuichezea Nkana na Namungo ya Tanzania, timu nyingine alizowahi kuzichezea ni Prisons Leopards ya Zambia na LLB Academic ya kwao Burundi, akipigiwa hesabu na miamba hiyo kutokana na uzoefu mkubwa alionao hadi sasa.