Mwalimu achukua nafasi ya Sopu AFCON

WAKATI kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kikiendelea na maandalizi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi amefanya mabadiliko kidogo ya kikosi.

Gamondi awali aliita wachezaji 28 watakaokwenda kushiriki fainali hizo zitakazoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, katika nyota hao, alikuwepo Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambaye sasa ametolewa, nafasi yake imechukuliwa na Seleman Mwalimu.

Taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyotolewa leo Desemba 13, 2025, imesema sababu za mabadiliko hayo ni baada ya Sopu kuumia.

“Kocha Miguel Gamondi amemuita mshambuliaji Selemani Mwalimu kwenye kikosi cha Taifa Stars cha wachezaji 28 watakaocheza AFCON 2025 Morocco kuchukua nafasi ya Abdul Suleiman “Sopu” ambaye ameumia,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika fainali hizo, Taifa Stars imepangwa Kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda ambapo sasa ipo Misri ikipiga kambi ya maandalizi kabla ya kwenda Morocco kushiriki mashindano hayo kwa mara ya nne baada ya 1980, 2019 na 2023.

Taifa Stars itaanza dhidi ya Nigeria Desemba 23, kisha Desemba 27 ikichuana na Uganda, itamaliza makundi Desemba 30 dhidi ya Tunisia.