Shinyanga. Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) katika Wilaya ya Shinyanga yamelalamikia baadhi ya vifungu vya sheria za kodi vinavyowalazimisha kulipa kodi kama kampuni za kibiashara, ingawa miradi yao inatoa huduma kwa jamii.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 13, 2025, na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGo) wilayani humo, Lucas Maganga, wakati akisoma risala kwenye kikao cha robo mwaka kuanzia Septemba hadi Desemba 2025.
“Licha ya Serikali kututatulia changamoto tofauti zilizokuwa zikitukabili awali, bado tunakabiliwa na changamoto kadhaa na tunaomba zitatuliwe, ikiwamo ya utozwaji kodi kubwa kama kampuni za kibiashara, pamoja na ugumu na urasimu wa kupata Charitable Status (hadhi ya hisani) kutoka TRA,” amesema.
Pia, amependekeza: “Tufanye mapitio ya pamoja ya miongozo ya TRA ili kutofautisha miradi ya kijamii isiyo ya kibiashara na shughuli zenye mapato, pamoja na TRA ianzishe dawati maalumu la kushughulikia masuala ya mashirika ngazi za wilaya na mkoa ili kurahisisha kufuatilia maombi ya misamaha ya kodi.”
Kwa niaba ya mashirika hayo, Maganga ameomba ushirikishwaji wa wadau wa NGOs wakati wa marekebisho ya sera na sheria za kodi ili kuleta uelewa wa pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima, kupunguza ngazi za idhini, na kuweka utaratibu wa kituo cha pamoja cha huduma (one-stop center) ili kurahisisha mchakato wa kupata ‘Charitable Status’.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameyapongeza mashirika hayo kwa kuendelea kufanya kazi za kuhudumia jamii na kuahidi kufanyia kazi changamoto zao, huku akitoa ushauri wa kisheria kwa mashirika hayo.
“Changamoto zilizotolewa hapa tunazichukua na kuzifanyia kazi, na nashauri anzisheni mawasiliano rasmi katika eneo la sheria, yatakayosaidia kuweka sawa migogoro ya kisheria. Pia, ongezeni juhudi katika kuhuisha mipango ya kazi ili iwe ya uhakika na yenye tija,” amesema Mtatiro.
“Pia, itasaidia kupanua wigo wa maeneo ya kuhudumia wananchi, kuongeza juhudi za utendaji kazi, na kuhakikisha wingi wa mashirika yaendane na tija, huku mashirika yasiyo na tija yafutwe,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mtatiro amesema: “Kuanzia mwaka 2026, mashirika yasiyo ya kiserikali, mbuni na kutafuta miradi ya kudumisha amani, usalama, utengamo, na ushauri kwa vijana katika maeneo hayo, yatapewa ufadhili mkubwa; ni miradi ambayo imekuwa ikipewa kipaumbele.”
