Pedro ataka mashine tatu Yanga, Dube ahakikishiwa maisha

KOCHA mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amekingalia kikosi cha timu hiyo kilivyo kwa sasa, kisha akatabasamu kabla ya kuuambia uongozi wa klabu hiyo, umletee mashine mpya tatu amalize kazi, huku akimwashia taa ya kijani mshambuliaji Prince Dube aliyeanza kuwa mtamu uwanjani.

Kama hujui, ni kama vile kocha Pedro anataka kutengeneza bomu litakalowalipukia na kuwasambaratisha wapinzani wa Yanga katika michuano inayoshiriki msimu huu ikiwa chini yake kwa kuwaambia mabosi wamtafutie watu watatu wa maana ili aje kukamilisha kuunda mziki anaoutaka.

Mabosi wa Yanga wamepokea ripoti ya kwanza wa Pedro baada ya kukisimamia kikosi hicho katika mechi sita za mashindano zikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na nne za Ligi Kuu Bara, zilizotosha kumpa picha ya wapi anataka kuiboresha mara michuano ikirudia tena.

Kwa sasa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikiwa Kundi B sambamba na Al Ahly ya Misri, JS Kabylie ya Algeria na AS FAR Rabat ya Morocco sambamba na Ligi Kuu Bara imesimama hadi mwisho mwa Januari ili kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

Taarifa kutoka kwa mabosi wa Yanga ni kwamba, Pedro ametaka kutafutiwa kiungo mkabaji mwenye ubora mkubwa, japo amesisitiza Duke Abuya amefanya kazi bora eneo hilo lakini anataka kumhamisha.

Ripoti ya Mreno huyo inasema, endapo atapata kiungo huyo mkabaji basi Abuya atahamishwa nafasi akisogezwa juu, hatua ambayo itaifanya Yanga kuwa na ubora mkubwa eneo la katikati kutokana na uwezo wa Mkenya huyo sambamba na kiungo atakayekuja.

Ripoti hiyo pia inahitaji kiungo mshambuliaji, yaani namba 10 na bado Pedro haridhishwi saana na watu alionao eneo hilo huku akionyesha hataki kutumia fundi Pacome Zouzoua eneo hilo.

Pedro ameonyesha anataka kumtumia Zouzoua kama kiungo wa pembeni akitokea kushoto akicheza eneo nusu (half space) jukumu litakalomfanya kuwa hatari zaidi mbele ya lango la mpinzani na kuinufaisha Yanga kuliko ilivyo sasa akiwa amefunga mabao mawili na asisti mbili vilevile.

Akili hiyo ya Pedro ya kutaka namba 10 inawaweka mtegoni Mamadou Doumbia na Lassine Kouma ambao walikuwa wanapewa nafasi kwa nyakati tofauti kucheza nafasi hiyo, licha ya Ecua Celestine naye kuwa mchezaji wa nafasi hiyo, japo kwa sasa anachezeshwa pembeni kama winga.

Kocha huyo Mreno pia anataka kutafutiwa winga mmoja mwenye ubora mkubwa atakayeongeza nguvu ya kuzalisha mashambulizi kutokea pembeni.

Kocha Pedro amewahakikishia mabosi wa Yanga hana shida na uwezo wa mshambuliaji, Prince Dube na anaamini endapo wachezaji hao wengine anaowataka watapatikana, kutampa urahisi Mzimbabwe huyo kuwa hatari zaidi.

“Tumeshaanza muda mrefu kuifanyia kazi hiyo ripoti na tunatafuta watu wa maana kweli, kama tukiwapata tunaona kabisa tutarudi kwenye mashindano msimu ujao tukiwa imara sana,” amesema bosi mmoja wa juu kutoka ndani ya Yanga.

Yanga kwa sasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 16 kupitia mechi sita, lakini inakamata nafasi hiyo katika Kundi B la Ligi ya Mabingwa nyuma ya Al Ahly ikivuna pointi nne kutokana na mechi mbili ilizocheza ikifunga AS FAR Rabat kwa bao 1-0 na kutoka suluhu na JS Kabylie na mapema mwakani itacheza mechi mbili mfululizo dhidi ya Al Ahly.