Dar es Salaam. Raia wa Bulgaria, Eduardl Mladenov (32) na Mtanzania Juma Ndambile (58) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka sita yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa na kujihusisha na miamala ya kutoa fedha zenye thamani ya Sh364 milioni kutoka benki za CRDB na NBC.
Pia, wanadaiwa kukutwa na mali ya wizi ambayo ni mashine ya kuchanjia kadi kwa ajili ya kufanya malipo ya fedha kwa njia ya kielekroni (POS) yenye thamani ya Sh500,000 mali ya Selcom Tanzania.
Washtakiwa hao wamefikishwa hapo jana Ijumaa, Desemba 12, 2025 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.
Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele akishirikiana na Winiwa Kassala, alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 29134 ya mwaka 2025.
Mshtakiwa Juma Ndambile (mwenye kofia nyekundu) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya uhujumu uchumi. Picha na Hadija Jumanne
Mwakamele alidai shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Alidai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati Januari Mosi, 2025 hadi Novemba 11, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wakiongoza genge la uhalifu wa kupangwa na kujipatia fedha.
Shtaka la pili ni kupatikana na mali ya wizi, linalomkabili Ndambile pekee yake, ambapo anadaiwa Oktoba 24, 2025 eneo la Mbweni, Wilaya ya Kinondoni alikutwa na mashine ya kuchanja kadi kwa ajili ya kufanya miamala ya fedha(POS) yenye thamani ya Sh500,000 mali ya Selcom Tanzania.
Shtaka la tatu ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu linayowakabili washtakiwa wote, ambapo kati ya Julai Mosi, 2025 hadi Novemba 11, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa kwa pamoja walidanganya na kujipatia Sh116 milioni kutoka NBC.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo, shtaka la nne, pia, ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, shtaka linalowakabili washtakiwa wote ambapo katika tarehe hizo na ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa udanganyifu wao walijipatia Sh248 milioni kutoka benki ya CRDB PLC.
Wakili Mwakamele aliendelea kudai kuwa shtaka la tano na la sita ni utakatishaji fedha na linawakabili washtakiwa wote wawili.
Alidai katika tarehe hizo, washtakiwa kwa pamoja walijusisha na miamala ya moja kwa moja ya kutoa pesa za kitanzania Sh116 milioni kutoka NBC na Sh248 milioni kutoka CRDB PLC, wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Mhini aliwaeleza kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi bali kwa kibali maalumu.
“Pia, hapa mna mashtaka mawili ya kutakatisha fedha ambayo yanawanyima nyie kupata dhamana, hivyo mtaendele kubaki mahabusu (gerezani) hadi hapo upelelezi utakapokamilika na kesi yenu kuhamishiwa mahakama ya juu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi,” alisema Hakimu Mhini.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hadi Desemba 23, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi umekamilika au laa na washtakiwa wamerudishwa rumande hadi terehe hiyo.
