Singida yaingia mazima kwa Lanso

BAADA ya Singida Black Stars kumrudisha Joseph Guede aliyekuwa anaichezea Al-Wehdat SC ya Jordan kwa mkopo, kwa sasa inaelezwa mabosi wa kikosi hicho wamemalizana na beki wa kulia wa KMC, Abdallah Said Ali ‘Lanso’.

Guede aliyejiunga na Singida Julai 2024, akitokea Yanga, aliitumikia timu hiyo kwa miezi sita, kisha kujiunga na Al-Wehdat ya Jordan kwa mkopo, kwa sasa amerejea tena kukitumikia kikosi hicho kuanzia Januari 2026.

Baada ya kumrejesha mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, Singida Black Stars inaendelea kuimarisha kikosi chake na sasa taarifa zinasema imemchukua Lanso ambaye awali waliikosa saini yake usajili uliopita wa dirisha kubwa.

Beki huyo aliyejiunga na KMC Januari 13, 2024, akitokea Mlandege, mkataba wake na kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni unafikia tamati Januari 2026, huku akigoma kuongeza muda wa kuendelea kusalia klabuni hapo, jambo lililotoa nafasi kubwa na nzuri kwa mabosi wa Singida kumsajili akiwa mchezaji huru.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, kimeiambia Mwanaspoti Lanso amemalizana na Singida Black Stars kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu.

“Ni kweli amesaini mkataba wa miaka mitatu, ataitumikia Singida kuanzia mwezi Januari na kama timu itashiriki Kombe la Mapinduzi basi ataungana na timu Kisiwani Zanzibar na ndiyo utakuwa mwanzo wa kuanza kuitumiki.

“Lanso alikuwa na ofa nyingi, Simba pia ilionyesha nia ya kumuhitaji, lakini Singida walikuwa wamewekeza nguvu hawajataka kuchelewesha mpango huo, wamekaa naye mezani na kumalizana naye haraka,” kimesema chanzo hicho.

Wakati huohuo, taarifa kutoka uongozi wa Singida, uliliambia Mwanaspoti, Lanso ni miongoni mwa mabeki wazuri na wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi zaidi, ingawa suala la usajili wake hawawezi kulizungumzia kwa sasa.

Kwa upande wa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka amesema hana taarifa za kuondoka kwa nyota huyo, ingawa kama kutakuwa na jambo lolote linalowahusu watalitolea ufafanuzi pale tu watakapoona inafaa wao kufanya hivyo.