Dodoma/Dar. Wakati mwili wa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, ukiagwa mjini Dodoma, Bunge limetaja chanzo cha kifo chake huku Rais Samia Suluhu Hassan akieleza sababu za kumwita kiraka.
Mbali na hayo, viongozi wa dini wamezungumzia kwa undani maisha yake ya kiroho, wakieleza namna alivyojitoa kulitumikia Kanisa.
Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, 2025, mwili wake umeagwa leo Desemba 13, 2025, baada ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, akisoma wasifu wa marehemu, amesema: “Jenista Mhagama alifariki dunia Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, kutokana na maradhi ya moyo.”
Mwili wa marehemu utazikwa Jumanne, Desemba 16, 2025, katika Kijiji cha Ruanda, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza kanisani hapo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema alimpa jina kiraka Mhagama kutokana na utendaji wake, akieleza kila alipompa jukumu alifanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Amesema Mhagama aligusa maisha ya wengi, akimwelezea kuwa alikuwa kiongozi jasiri, mlezi wa wengi ndani ya Bunge na Serikali, aliyejitoa kuwatumikia wananchi.
“Alisimama imara kutetea watu aliowaongoza, alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na viongozi. Alikuwa mfano wa uongozi uliotawaliwa na uadilifu, nidhamu na hofu ya Mungu,” amesema na kuongeza:
“Nashukuru Mungu leo ndani ya kanisa hili nimepata kuyajua maisha yake ya kiroho na kidini. Awali nilimfahamu zaidi kwa maisha yake ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi.”
Samia amesema Mhagama alikuwa mwalimu kitaaluma na mwalimu wa uongozi, aliyetumia kipawa chake kulea na kusimamia mawaziri akiwa Mnadhimu, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na Mwenyekiti wa Bunge.
Amesema wabunge na mawaziri walimheshimu, naye alijiheshimisha katika nafasi zake, akitoa mchango mkubwa kwa chama, Bunge na Baraza la Mawaziri.
“Yeye ni mtu pekee katika historia ya nchi aliyeweza kuvaa kofia mbili kwa wakati mmoja, ikiwemo Katibu wa Kamati ya Chama cha Mapinduzi na Mnadhimu wa Serikali bungeni. Kofia hizo zilimtosha na kumuenea sawasawa,” amesema.
Amesema hakuwa mtu wa mzaha, lakini alikuwa mcheshi, mtii kwa mamlaka, chama chake na wananchi wake.
“Alikuwa mnyenyekevu kwa Mungu wake, mambo yaliyomfanya apendwe na kuheshimiwa na watu walio chini yake pamoja na viongozi wenzake,” amesema.
Amesema alipofanya kazi chini ya uongozi wake kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Waziri wa Afya, alimpa jina kiraka kwa sababu kila alipomweka aliziba vizuri.
“Alikuwa kiongozi anayesimama imara kutetea masilahi ya nchi bila kuchoka na bila kujali changamoto. Kupitia sauti yake bungeni, mchango wake katika jamii na msimamo wake katika uongozi, ameacha kumbukumbu njema na kuandika historia nzuri kwa ajili yake,” amesema na kuongeza;
“Wabunge na mawaziri, hususan wale wapya, niwaase kufuata nyayo zake, kwani mafanikio ya Bunge na Taifa yanatokana na mshikamano wa wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa.
“Mijadala inabaki katika misingi ya kistaarabu na kuhakikisha inalinda heshima ya Bunge kama chombo cha uwakilishi na wananchi na kutimiza wajibu wenu kwa uadilifu kama alivyokuwa Jenista Mhagama.”
Amesema safari yake ya uongozi haikuwa rahisi, lakini aliitembea kwa ujasiri, hekima na heshima.
“Tunapomuaga, tunabaki na kumbukumbu za tabasamu lake. Niliwahi kuwasikia watu wakisema Jenista hajawahi kukasirika, ukweli ni kwamba, alikuwa anakasirika lakini wakati wote alikuwa anatabasamu. Tutalimisi tabasamu lake, lakini pia moyo wa kujali masilahi ya Taifa,” amesema.
Awali, Paroko wa Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Padri Emmanuel Mtambo amesema mbali na utumishi wa Serikali na nyanja za kisiasa, Mhagama alikuwa mtumishi mwaminifu ndani ya kanisa.
Amesema alikuwa mfano wa utumishi na utoaji wa zaka na misaada kwa wasiojiweza, akieleza mara nyingi alikuwa akitoa sadaka lakini hakutaka atangazwe.
“Mara kadhaa alikuwa akimtuma dereva wake kuleta sadaka hiyo, lakini alikataa kutangazwa hadharani na ndivyo tulivyofanya,” amesema.
Ameeleza hata vazi alilovaa wakati wa misa na kitambaa kilichotandikwa altareni ni vipya ambavyo vilitolewa kwa kanisa na Mhagama.
Amesema amesaidia katika ujenzi wa minara na uwekaji wa sanamu kubwa ya Bikira Maria ambayo imejengwa eneo la kuingia kwenye kanisa hilo.
Victor, mtoto wa marehemu, amesema wakati wengine wakimuita Jenista kiongozi, wao walimuita mama na katekista kwa sababu alikuwa mwalimu wa dini nyumbani.
“Tulimpenda sana mama, tuliishi naye kwa karibu na kwa upendo, naye aliunganisha familia yetu,” amesema.
Amemshukuru Rais Samia akisema mama yake alipougua walitoa taarifa na kwa muda mfupi walisaidiwa haraka hadi kufika Hospitali ya Benjamin Mkapa ambako mama yao alihitimisha safari ya maisha yake duniani.
“Kwa kweli tunashikilia yale maneno uliyokuwa unayasema kila siku, ‘mama huyu ni kiraka’ na ulisema unamtumia sehemu nyingi sana. Ulipofika siku ile Peramiho nyumbani ukasema ‘libarikiwe tumbo lilomzaa Jenista Mhagama’.
“Kwa wachache wasioelewa, ulimaanisha nini, mama yetu huyu ametokana na mama Epifania Ngonyani, ambaye ni muasisi wa UWT Taifa na mwenyekiti wa kwanza wa UWT Mkoa wa Ruvuma,” amesema na kuongeza:
“Amehudumu kwa miaka 25, katika imani, katulea katika misingi ya kupenda nchi, katulea katika chembechembe ya uongozi, hivyo tumechipukia na mama yetu alichipukia humo mpaka akasimama.”
Amesema mama yao alikuwa na sifa za kipekee, kwani hata siku za sikukuu alikwenda kazini na alipoulizwa kwa nini alisema asipojenga nchi, nani atajenga na akawataka wamsaidie Rais kufanya kazi.
“Mama aliamini katika kuchapakazi, alitusihi wote tupende nchi yetu, tuwe wazalendo, tuchapekazi hakuna namna nyingine, alitusihi wote tuliopita kwenye mikono yake, uchaji wa Mungu, elimu pia kwa sababu alipenda kusoma, hivyo nyumbani vilijaa vitabu,” amesema.
Amewasihi Watanzania kuenzi maisha yake kwani alijali utu na fadhila, hakujali mkubwa wala mdogo, masikini wala tajiri bali aliwasimamia kwa haki na upendo.
“Ushuhuda wa wengi waliojaa humu waliguswa na maisha ya mama na walimfahamu katika nafasi mbalimbali, ninawaomba tuendelee kuishi katika ukristo wake na tukikumbuka kuwa, Jenista Mhagama aliipenda nchi na wana Peramiho,” amesema.
Amesema kwa kushirikiana na Serikali miradi mingi imekwenda Peramiho ikiwemo shule, zahanati, barabara, huku akisema mama yake hana deni na amewasitiri wana Peramiho.
“Hata mkifanya buriani mkiangalia uso wake umejaa tabasamu kwa sababu njia aliyoipita ni salama, tuipite pia katika imani, ushirikiano na maendeleo,” amesema.
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema katika miaka 25 ya ubunge wa Mhagama, wananchi wa Peramiho hawana malalamiko juu yake.
Amesema alikuwa mtumishi wa kweli kwa watu wake, alikuwa mnyenyekevu na aliwapenda watu wake.
“Katika kipindi chote cha utumishi alitanguliza mbele kuwatumikia wananchi waliomchagua na hata alipokuwa waziri hakuacha kazi hiyo, huku akiguswa na wanyonge,” amesema na kuongeza:
“Ndiyo maana leo wanyonge wa Peramiho wana uchungu kuliko mtu yeyote kwa sababu wanajua mpiganaji wao, mtetezi wao ameondoka, ametangulia mbele za haki. Ni ombi letu kuwa wapate mtumishi mwingine wa aina yake.”
Amesema wakati akitafakari kifo cha mbunge huyo aliwaza kama Mungu angemwambia aombe jambo moja, angeomba wabunge wote wa CCM na madiwani wapende na kutumikia watu kwa kiwango cha Jenista.
“Tumeletwa duniani si kuishi tu, bali kutumikia wenzetu. Ni utumishi kwa binadamu wenzetu unaotupa heshima mbele ya Mungu na watu watukumbuke kwa kazi zetu tulizofanya,” amesema.
Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema Mhagama alikuwa kiongozi aliyeipenda nchi yake kwa dhati na aliyekuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge na kiuongozi.
Amesema tangu aingie bungeni mwaka 2005 alimzoea Mhagama akimwita mwanaye, naye akimwita mama.
“Sifa zote zilizotolewa hapa ni za ukweli. Ni mtu aliyejishusha sana. Kikubwa ni kumuombea Mungu ampokee na amuweke pema, yeye na wengine waliotangulia mbele za haki,” amesema.
Amemshukuru Rais Samia kwa namna alivyokuwa karibu na Bunge wakati wa msiba huo, pamoja na kutoa ndege kwa ajili ya kupeleka mwili wa Mhagama Songea.
