SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa adhabu ya kuwapokonya pointi tatu klabu za Bunda Queens na Tausi baada ya kushindwa kufika uwanjani kwenye mechi za kwanza za Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu 2025-2026.
TFF imethibitisha kuwa, timu hizo zilikiuka Kanuni ya 32 ya Ligi ya Wanawake (2025) baada ya kutofika kucheza mechi zilizopangwa Desemba 8, 2025.
Katika mechi namba 01, Bunda Queens ilitakiwa kuumana na JKT Queens kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, lakini ilishindwa kufika uwanjani, hatua iliyowapa Wanajeshi hao ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu.
Mbali na kupoteza mechi hiyo kikanuni, Bunda Queens imekatwa pointi tano na kutozwa faini ya Sh5 milioni, huku mwenyekiti wa klabu hiyo akifungiwa mwaka mmoja.
Kwa upande wa Tausi iliyoshindwa kufika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya Mashujaa Queens, timu hiyo imepewa adhabu sawa na Bunda Queens ambapo ni kukatwa pointi tano, faini ya Sh5 milioni na mwenyekiti wa klabu kufungiwa mwaka mmoja. Mashujaa Queens imepewa ushindi wenye mabao 3-0.
Kanuni ya 32 katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kuhusu Kutofika Uwanjani, inafafanua kwa kina adhabu hizo.
(1) Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo: 1.1 Itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na magoli matatu (3).
1.2 Kutozwa faini isiyopungua shilingi milioni tano (5,000,000/=) ambapo 50% ya faini itachukuliwa na TFF na 50% italipwa kwa timu pinzani. 1.3 Kulipa fidia ya maandalizi/ualibifu wowote unaoweza kujitokeza.
1.4 kupokwa alama tano (5) katika msimamo wa Ligi pamoja na Mwenyekiti au Rais wa Klabu kufungiwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja (1) hadi mitano (5).
1.4.1 Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya tano (5), itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo wa Ligi.
1.4.2 Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa Ligi ya hadhi yake.