Ulega awaonya mameneja wa Tanroads wasiozingatia maslahi ya vijana

Mbeya. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema meneja yeyote wa Tanroads ambaye mradi hautanufaisha vijana wa eneo husika atakuwa shakani kuendelea na nafasi yake.

Ulega ametoa kauli hiyo leo, Desemba 13, 2025 wakati akikagua ujenzi wa daraja la Nsongwe lililopo wilayani Mbeya, baada ya kupokea kilio cha vijana walioeleza mradi huo kutowanufaisha upande wa ajira.

Akiwakilisha vijana wengine wa Kata ya Bonde la Songwe, Joseph Lendela amesema wanaishukuru Serikali kwa kujenga daraja hilo, ambalo litamaliza changamoto ya mafuriko kwa wananchi.

Amesema pamoja na neema hiyo, mradi huo tangu kuanza hadi sasa unapofikia tamati, vijana wa eneo hilo hawakunufaika kwa lolote, badala yake walibaki kuhangaika.

“Tunashukuru ujio wako Waziri (Ulega). Huu mradi una faida kubwa kwetu wananchi, lakini kilio chetu vijana ni ajira. Hili daraja liko hapa, ila cha kusikitisha hakuna mwenyeji aliyenufaika, unataka tuibe?” amehoji Lendela.

Akijibu kilio hicho, Waziri Ulega amesema jambo la ajira kwenye ujenzi wa barabara si la wakandarasi, kwa kuwa hawajui chochote, hivyo maslahi ya vijana yapo kwa meneja husika kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali kwa uwakilishi.

Amesema kila siku miradi ya ujenzi wa barabara inakuja, hivyo vijana wa kila eneo husika wanapaswa kupewa kipaumbele, na wanapomaliza wapewe vyeti kama kutambua mchango wao pamoja na ujuzi na maarifa waliopata.

“Mameneja… nawaita mara tatu. Rais Samia anataka katika kila mradi ambao fedha zinatoka serikalini, vijana wapewe kipaumbele. Kila nitakapokuwa nakagua mradi, nauliza viongozi wa eneo na vijana wenyewe kujua wamenufaikaje.

“Vinginevyo, meneja yeyote ambaye hasimamii maslahi ya wanaotutuma hizi kazi atakuwa kwenye mashaka, kwa kuwa itakuwa sehemu ya kukupima maksi ya kukufanya kuendelea kuaminika; haya ndiyo Watanzania wanataka,” amesema Ulega.

Waziri huyo ameongeza kuwa wakati daraja hilo likikamilika Desemba 28, 2025, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Suleiman Bishanga, aangalie uwezekano wa kuruhusu maegesho ya malori katika eneo hilo linapobaki ili kufungua shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Kuhusu changamoto za barabara zilizowasilishwa na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Patali, Ulega amesema Meneja wa Tanroads atatoa ripoti na tathmini baada ya ziara yake, kisha kuwasilisha wizarani.

“Kama kuna ambacho kipo nje ya uwezo wake, atawasilisha kwangu, lakini nampa baraka suala la maegesho ya malori ili kuifungua Mbeya Vijijini kiuchumi. Pia, hizi taa ziwekwe vizuri katika maeneo ya shughuli za wananchi,” amesema Ulega.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanroads mkoani humo, Bishanga, amesema daraja hilo linatarajiwa kukamilika Desemba 28, 2025, na limegharimu Sh9.5 bilioni.

“Ni daraja la mita 30 ambalo linajengwa na kampuni ya CICO ya China. Linagharimu Sh9.5 bilioni na linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, na litamaliza changamoto iliyokuwapo,” amesema meneja huyo.