Cameroon. Watu wanane wamefariki dunia kutokana na moto uliolipuka baada ya lori la mafuta kufeli breki kwenye mteremko katika Jiji la Douala nchini Cameroon.
Maofisa wa kikosi cha Zimamoto walilazimika kuzima moto kwa siku nzima jana Ijumaa Desemba 12, 2025 kutokana na kuongezeka kwa kasi kutokea kwenye lori hilo ambalo lilikuwa limebeba zaidi ya lita 36,000 za mafuta.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka za usalama na nchini humo zinasema kuwa moto huo ulilipuka baada ya lori hilo kupata hitilafu kwenye mfumo wa breki katika kilima cha Mutengene. Hivyo liliteremka mlima kwa kasi na mwishowe kuanguka jirani na daraja la Likomba, eneo la Tiko.
Mlipuko huo wa moto iliwazimu wakazi wa eneo ilipotokea ajali kukimbia ili kuokoa maisha yao. Takriban nyumba 10 na magari kadhaa yaliyokuwepo jirani nayo yalitetekea moto.
Taarifa ya awali inaeleza kuwa waliopoteza maisha ni wanaume, wanawake pamoja na mtoto mmoja, ambapo miongoni mwao wameungua jambo lililosababisha kushindwa kutambulika kwa urahisi.
“Msimamizi wa Maafa wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika mji wa Limbe, Okwandum Samuel Ndenzen amenukuliwa akisema, “Hatuwezi kuthibitisha kama idadi ni hiyo iliyotajwa pekee ya watu wanane, kwa sababu magari bado yapo hapo, lakini tunaendelea kakagua kila mahali iwapo tutawapata wengine.”
Manusura watatu waliopata majeraha waliwahishwa katika Hospitali ya Bingo, huku wanajeshi kadhaa waliopata majeraha madogo wakati wa uokoaji pia walipatiwa matibabu.
Serikali ya Jiji la Douala ilituma kikosi cha ziada cha wazima moto. Vilevile barabara kuu katika eneo hilo ilifungwa kwa muda ili kupunguza msongamano wa magari.
