Morogoro. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo, amewataka wahitimu wa Chuo cha Ardhi Morogoro kujiepusha na vitendo viovu vinavyolenga kuharibu amani ya Taifa la Tanzania.
Pia, amewataka wahitimu hao kuwa wazalendo kwa Taifa na kuepuka vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyosababisha baadhi ya watu kukosa haki zao za msingi, hatua inayochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya kudumu katika jamii.
Akwilapo amesema hayo Desemba 12, 2025, katika mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Amesema ni vema wahitimu hao wakatumia elimu na maarifa waliyopata chuoni hapo kwa manufaa ya jamii na kupunguza migogoro ya ardhi nchini, ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa wakati wa utekelezaji wa majukumu ya sekta ya ardhi, hatua itakayosaidia kuepuka migogoro katika jamii.
“Tumieni utaalamu wenu kwa weledi na uadilifu mkifuata kanuni na sheria zilizowekwam, epukeni kabisa vitendo vya rushwa, mkikumbuka kuwa rushwa ni adui wa haki katika jamii,” amesema Akwilapo.
Katika hatua nyingine, Akwilapo amewatahadharisha wahitimu hao kutokubali kuingia katika mkumbo wa kufanya vurugu zinazochochewa kupitia mitandao ya kijamii, ikilenga kuleta machafuko hapa nchini kwa lengo la kulirudisha nyuma Taifa la Tanzania.
“Sasa kuna vijana wengine wameingia katika mkumbo huo ovu, wanaitwa Gen Z, hawasikilizi, hawaambiliki. Nawasihi msingie katika uovu huo. Hii ni mbinu iliyotengenezwa ili kuleta machafuko katika nchi zinazoendelea ili wao wafaidike mnapogombana,” amesema Akwilapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema chuo hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kupanga, kusimamia na kuendeleza matumizi bora ya ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kupitia wataalamu wanaozalishwa chuoni hapo.
Aidha, katika risala iliyosomwa na rais wa chuo hicho, Faraja Samweli, imebainishwa kuwa chuo kinakabiliwa na changamoto zinazohitaji msaada na uangalizi wa hali ya juu kutoka serikalini, ikiwamo upungufu wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia kama vile ukosefu wa studio ya kisasa ya mipango miji na maabara ya kompyuta isiyokidhi idadi ya wanafunzi.
Chuo cha Ardhi Morogoro kilianzishwa mwaka 1958 kikiwa na lengo la kutoa elimu ya mafunzo katika kozi za Geomatikia (Geomatix), Mipango Miji na Vijiji (URP) na Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS).
Kwa mwaka 2025, jumla ya wanafunzi 450 wamehitimu katika ngazi ya astashahada na stashahada.
