WAZIRI SANGU: MFUMO e-UTATUZI MAFANIKIO MAKUBWA CMA

Na: Ofisi ya Waziri Mkuu – KAM

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa mafanikio makubwa katika utatuzi wa migogoro ya kikazi, baada ya kusuluhisha migogoro 4,339 hadi kufikia Septemba 2025.

Waziri Sangu ametoa pongezi hizo Desemba 13, 2025, jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, ziara inayolenga kufahamu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo, kuimarisha uhusiano wa kikazi, pamoja na kutoa maelekezo yatakayoongeza ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na Menejimenti ya CMA Mhe. Sangu ameitaka Tume kuendelea kukuza matumizi ya teknolojia katika utatuzi wa migogoro ya kikazi, hususan kuboresha na kuimarisha matumizi ya Mfumo wa e-Utatuzi.

Aidha, ameagiza kuwekwa kwa mazingira rafiki ya matumizi ya mfumo huo ili uweze kutumika kikamilifu kama nyenzo madhubuti ya kumaliza migogoro sehemu za kazi kwa haraka na kwa ufanisi.

Awali, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, ameisisitiza CMA kuendelea kujitangaza na kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa na Tume, sambamba na kuimarisha misingi ya usawa na haki mahala pa kazi.

Vile vile, amewahimiza watumishi wa Tume kuzingatia usuluhishi kama njia muhimu ya kutatua migogoro ya kikazi, akisisitiza kuwa mazungumzo huchangia utoaji wa haki kwa wakati na hupunguza migogoro kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Usekelege Mpulla, amesema Tume itaendelea kuboresha utendaji wake kwa kuwekeza zaidi katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma za utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (akiyesimama) akizungumza na Menejimenti ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi – CMA Disemba 13, 2025 Jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake,