Zitto ashida kesi dhidi ya Harbinder Sethi wa IPTL

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeitupilia mbali kesi ya madai ya zaidi ya Sh15 bilioni iliyofunguliwa na mfanyabiashara, Harbinder Sethi dhidi ya Zitto Kabwe.

Katika shauri hilo, Sethi alidai ndiye mwenye hisa nyingi katika Kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP) iliyosajiliwa Tanzania na kwamba, PAP inamiliki pia Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Zitto, mwanasiasa aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, alifunguliwa kesi ya madai ya kumkashifu Sethi kupitia ukurasa wake wa Twitter sasa X, Aprili 4, 2025.

Katika hukumu aliyoitoa Desemba 11, 2025 na kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama leo Desemba 13, Jaji Arnold Kirekiano, amesema mwombaji hajathibitisha kesi kwa kiwango kinachohitajika, hivyo shauri hilo linatupiliwa mbali na atatakiwa kulipa gharama za kesi.

Zitto katika ukurasa huo aliandika: “Kwanza naunga mkono msimamo wa uongozi wa Shirika la Tanesco kwamba imekwishamalizana na IPTL na hivyo haina madai yoyote kutoka kwa tapeli yeyote anayejiita mmiliki wa IPTL.”

“Hivyo basi kitendo cha Bwana Sigh Sethi kuendelea kudai kumiliki IPTL na kuisumbua Serikali na Tanesco ni utapeli wa wazi kwa kuwa hautokani na sheria wala amri yoyote ya mahakama.”

Zitto aliandika: “Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) wanapaswa kufuta usajili wa Kampuni ya IPTL na takataka zingine zote zinazohusiana na IPTL. Mzoga huu sasa uzikwe.”

Kutokana na andiko hilo, Sethi akafungua shauri la madai ya kashfa dhidi ya Zitto akidai matamshi hayo yalitolewa kwa nia mbaya, bila sababu au uhalali wa kisheria. Pia yalimweka katika chuki, dharau na kejeli kutoka kwa umma, wawekezaji wengine na jamii yake.

Madai ya fidia, majibu ya Zitto

Katika shauri namba 8810 la mwaka 2025, Sethi aliiomba mahakama itamke kuwa Zitto alimkashifu ma kwamba, matamshi na chapisho lake ni la uongo na lenye madhara.

Aliiomba mahakama imwamuru Zitto amuombe radhi bila masharti na kuondoa uchapishaji wa uongo na ovu wa kukashifu anaoulalamikia kupitia jukwaa lilelile alilolitumia la Twitter.

Vilevile, aliiomba mahakama imwamuru achapishe tangazo la kuomba radhi bila masharti katika magazeti ya Mwananchi na Daily News kwa wiki nzima kwa maandishi makubwa, ukurasa wa kwanza.

Sethi aliiomba mahakama pia imwamuru kutoa matangazo ya kuomba radhi kupitia televisheni na redio maarufu nchini kwa wiki nzima.

Vilevile, aliiomba mahakama imwamuru Zitto kumlipa Sh10 bilioni zikiwa ni fidia ya kashfa na uharibifu wa upotevu wa sifa uliosababishwa na matamshi hayo.

Pia, aliomba mahakama imwamuru Zitto amlipe hasara ya jumla ya kashfa ya Sh5 bilioni na kumsababishia madhara makubwa ya msongo wa mawazo kwa sababu ya uchapishaji wa kashfa na nafuu yoyote ambayo mahakama itaona.

Sethi aliwakilishwa na mawakili Dorah Malaba na Musa Mhagama, huku Zitto akiwakilishwa na mawakili Moses Mgonja na Anita Nyangahondi.

Zitto aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), alikana kufanya jambo lolote baya akieleza aliyochapisha ni ya kweli, aliyatoa kwa nia njema na ni maoni ya haki kuhusu masuala yenye masilahi makubwa ya umma.

Alihusisha maoni yake na haki ya uhuru wa kujieleza, akakana madai ya nafuu iliyoombwa, akiiomba mahakama kufuta shauri hilo.

Katika kuamua shauri hilo, hoja nne ziliandaliwa, moja ikiwa iwapo maneno yaliyochapishwa na mjibu maombi yalikuwa ya uongo na yenye nia mbaya, pili kama machapisho hayo yalikuwa yamemkashifu mleta maombi.

Iwapo hoja hizo mbili ni za kweli, nyingine ambazo zilipaswa kuamuliwa ni kama mleta maombi alipata madhara yanayohitaji fidia na nini mahakama itoe kama nafuu kwa upande ambao utashinda kesi hiyo.

Sethi alirejea maudhui yaliyochapishwa na Zitto akaeleza matamshi yalikuwa ya kashfa kwake, washirika wake wa kibiashara na dini, kwani alionekana tapeli.

Alirejea shauri la maombi namba 49 la 2002 na 254 la 2003, yaliyoshughulikia suala la kumaliza shughuli (winding up) za IPTL.

Alieleza Mahakama ya Rufani, haikusema yeye si mmiliki wa IPTL na kumbukumbu za Brela zinaonyesha PAP ndiyo mwanahisa mkubwa wa IPTL.

Sethi alidai Zitto alitoa matamshi ya uongo kwa kuwa alitumika na Benki ya Standard Chartered Bank Hong Kong, ambaye ni hasimu wa PAP aliyodai ilinunua deni la IPTL, huko Malaysia.

Alidai alipata sifa nzuri kutoka Serikali ya Tanzania na Wizara ya Nishati, washirika wake wa kibiashara na jumuia ya kidini akieleza alikuwa kiongozi wa Sick Temple, mkoani Iringa yenye waumini 8,000.

Kwa upande wake, Zitto alieleza katika kipindi cha ubunge alihudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na POAC kwa miaka minane mfululizo na zilipewa jukumu la kuchunguza kashfa iliyohusisha IPTL na PAP.

Kashfa hizo ziliibuliwa bungeni kuhusu matumizi mabaya ya fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ni kupitia uchunguzi wa kamati alizoziongoza alimfahamu Sethi kuwa ana uhusiano na kampuni hizo mbili.

Alieleza machapisho yake katika mtandao wa kijamii aliyaandika na ilikuwa sehemu ya mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilijadiliwa bungeni.

Alieleza yeye kama mwananchi na mtu aliyefahamu vizuri suala hilo, alikuwa na haki na wajibu wa kutoa maoni kutokana na mjadala wa ripoti ya CAG, ambaye alizungumzia pia madai ya IPTL dhidi ya Tanesco.

Zitto alieleza maoni yake aliyatoa kwa nia njema kutoka kwa mtu aliyefahamu suala hilo, hivyo haliwezi kuhusishwa na madai ya kashfa na kwamba, maoni yake pia yaliegemea uamuzi wa mahakama uliotolewa na Jaji Utamwa.

Alieleza maoni yake yaliegemea katika wajibu wake kama raia kupitia ibara ya 27 ya Katiba ya Tanzania, juu ya wajibu wa kulinda rasilimali za umma, lakini pia kutumia haki yake ya kutoa maoni, kukemea wizi wa fedha za umma.

Jaji Kirekiano amesema ni jambo la kawaida kwamba mzigo wa uthibitisho uko kwa mlalamikaji anayefungua kesi, anayepaswa kuthibitisha madai.

Akirejea kesi iliyoelezwa na Sethi amesema katika uamuzi wa shauri hilo, hakuna uamuzi wa mahakama unaohusu umiliki wa IPTL.

Jaji alirejea matamshi yanayolalamikiwa yanayosema: “Hivyo basi kitendo cha Bwana Sigh Seth kuendelea kudai kumiliki IPTL na kuisumbua Serikali na Tanesco ni utapeli wa wazi kwa kuwa hautokani na sheria wala amri ya mahakama.”

Kwa ushahidi wa mleta maombi, amesema alijaribu kujenga kesi kuwa yeye ni mmiliki wa IPTL, hivyo madai kwamba Tanesco haina deni lolote kwa kampuni ya IPTL yalichapishwa kwa nia mbaya na kumfanya aonekane tapeli.

“Utegemezi ulifanywa katika uamuzi wa mahakama kwa maana hiyohiyo haikusema lolote kuhusu umiliki wa IPTL. Si wajibu wa mahakama hii kujibu madai ya umiliki wa mleta maombi ambao umebishaniwa sana,” amesema.

Jaji amesema: “Masilahi yangu ni kama, kwa kuzingatia uamuzi huo, mahakama hii inaweza kufuta kwamba mlalamikiwa atatoa maoni yake kuhusu mjadala wa kuwa ripoti ya CAG ilikuwa na nia mbaya dhidi ya mleta maombi kwa jina lake.”

Amesema amezingatia madai ya mleta maombi kuwa chapisho lilikuwa na nia mbaya na pia msimamo wa mjibu maombi kwamba maoni yake hayakuwa na hasidi ndani yake bali aliyatoa kwa haki na alikuwa na wajibu huo.

Jaji amesema ushahidi uliowasilishwa kortini kuhusu chapisho hilo lilihusu madai ya IPTL dhidi ya Tanesco ambayo ni taasisi ya umma.

“Kwa maelezo hayo, madai yoyote ya IPTL yanayodaiwa kumilikiwa na PAP ambayo tena inadaiwa kumilikiwa na mleta maombi ni jambo linalostahili kutupiwa jicho na umma,” amesema na kuongeza:

“Kwa uwazi, nimesema ‘inadaiwa’ kwa sababu wakati mwombaji alitaja rekodi kwa mujibu wa Brela, hakuna ushahidi kama huo uliotolewa.”

Amesema: “Katika hali hii ya ukweli, pamoja na ushahidi usiopingika kutoka kwa shahidi wa kwanza wa utetezi (Zitto) kwamba suala la umiliki wa IPTL lilikuwa ni suala la uchunguzi wa Bunge, suala hili kwa kiasi kikubwa lilikuwa ni la masilahi ya umma.”

Amesema amezingatia hoja ya wakili Malaba kwamba maoni ya wahojiwa hayawezi kuchukua nafasi ya uamuzi wa mahakama

“Hoja hii inazingatiwa, hata hivyo, kama ilivyodokezwa hapo juu, kwa kuwa Zitto alieleza kuwa alikuwa anatoa maoni yake, kwa hivyo, tafsiri yake inapaswa kuwa kamilifu maadamu ina msingi katika ukweli ambao ni kweli,” amesema.

Amesema mleta maombi hajathibitisha katika kiwango kinachohitajika kuwa chapisho lilikuwa la uongo na hasidi, hivyo hakukuwa na nia ovu na chapisho halikuwa la uongo.

Jaji amesema Sheria ya Huduma za Habari 2016 inasema chapisho linaweza lisiwe la kashfa kama suala lililoandikwa ni la kweli na lina masilahi ya umma.

Baada ya maelezo hayo, jaji amesema mleta maombi ameshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachokubalika, hivyo kesi inatupwa na atawajibika kulipa gharama.