Dar es Salaam. Mwanadiplomasia nguli wa Tanzania, aliyewahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Eswatini na Namibia, Timothy Bandora (72), amefariki dunia akiwa jijini Nairobi, nchini Kenya, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Bandora, ambaye aliitumikia Serikali kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tatu, alitekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika utumishi wa umma pamoja na ndani ya Umoja wa Mataifa (UN), akihudumu katika nyadhifa tofauti kwa uadilifu na weledi mkubwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya msiba iliyotolewa na familia, marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumanne, Desemba 16, 2025, katika Makaburi ya Kinondoni.
Ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa majukumu aliyofanya wakati wa uhai wake ni kuongoza kurugenzi ya ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ofisi ya Lagos, ambayo pia inahudumia nchi za Benin, Togo, Cote d’Ivoire, Ghana, Guinea, Senegal, Burkina Faso, Mali, Sierra Leone, Liberia, Guinea-Bissau na Mauritania.
Katika wigo wa kimataifa, Balozi Bandora aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, ambako alifanya kazi kwa miaka kadhaa.
Katika muda huo, alishiriki katika shughuli mbalimbali za usuluhishi wa migogoro barani Afrika, hasa katika kipindi ambacho bara hilo lilikabiliwa na migogoro mingi ya ndani, akichangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kudumisha amani na utulivu.
Atakumbukwa kwa kuhusika katika kubuni na kuandaa Mfumo wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika (AU Peace and Security Architecture) na pia alihusika kwa kiasi kikubwa katika kuandaa na kuanzisha Mpango wa Upimaji wa Utawala Bora Barani Afrika chini ya NEPAD (African Peer Review Mechanism – APRM).
Katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), mwanadiplomasia huyu pia atakumbukwa kwa kuhudumu kama mjumbe wa Kamati ya Kiufundi ya SADC iliyobuni Chombo cha Siasa, Ulinzi na Usalama cha SADC, ambacho mpaka sasa kina wajibu wa kukuza amani, utengamano na usalama miongoni mwa nchi wanachama.
Aidha kati ya kazi nyingine aliyopata kushiriki katika kubuni wa mfumo wa OAU, wakati huo sasa AU, wa kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro. Balozi Bandora alihudumu kama Mjumbe wa Kamati ya Kiufundi ya Mkutano wa Utulivu, Usalama, Maendeleo na Ushirikiano Afrika (CSSDCA), uliodhaminiwa na OAU, ECA na Africa Leadership Forum.
Alihudumu kama mjumbe wa kundi la wataalamu juu ya uthibitishaji wa majaribio ya nyuklia katika mpango wa nchi sita kuhusu amani na Maendeleo (Six Nations Initiative for Peace and Development) uliotekelezwa na Marais wa India, Argentina, Mexico, Ugiriki, Uswisi na Tanzania.
Katika nafasi hiyo, aliwahi pia kuwa mshauri wa kiufundi wa Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu masuala ya usitishaji wa silaha na udhibiti wa silaha; ni katika kipindi hicho pia alihudumu kama mjumbe wa kundi la wataalamu la Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo yasiyo na silaha za nyuklia.
Kazi zote hizi zilimfikisha Balozi Bandora katika majukumu makubwa zaidi ya kimataifa akihudumu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, akiwa Mkuu wa Masuala ya Utawala-Ofisi ya Afrika kabla ya kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Mratibu Mkazi (Resident Coordinator) wa Umoja wa Mataifa katika nchi za Eswatini (Swaziland) na Namibia ambako alihitimisha utumishi wake mwaka 2015, kwa kustaafu kwa heshima baada ya utumishi uliotukuka.
Balozi Bandora ameacha mjane, Margaret Bandora na watoto sita Rebecca, Semu, Tugwire Timothy Junior; Patrick (Chifu); Rhoda Mkazi, na Patricia Mhoja. Mungu pia alimbariki kuona wajukuu wake watatu, Marscha Kasamba, Tarai Kasamba na Michael Bandora.