Kigoma. Zaidi ya Sh53 bilioni zimetarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Hayo yamebainishwa leo, Desemba 14, 2025, na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kisena Mabuba, wakati wa ziara ya waandishi wa habari ya kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa na manispaa hiyo.
Amesema kuwa jumla ya miradi 57 imetekelezwa, huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi, ikilenga kuimarisha huduma na maendeleo ya jamii ndani ya Manispaa.
Mabuba amesema kuwa miradi yote imeshaanza kutekelezwa, na tayari baadhi yake imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, ikiwemo ofisi za watendaji wa kata na Hospitali ya Manispaa, ambayo pia tayari imeanza kutoa huduma.
Ujenzi wa kituo cha afya cha Rusimbi,Manispaa ya Kigoma ujiji kitachawasogezea huduma za afya wananchi wa kata za jirani na wenyeji wa kata ya Rusimbi.
Aidha, Mabuba ameleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo soko la kisasa la Mwanga litakalojengwa sambamba na Mwalo wa Katonga, litakayogharimu takriban Sh16 bilioni, litachangia kufungua uchumi wa manispaa kama lango la mkoa.
Pia, itasaidia kuchochea shughuli za biashara na uchumi, kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi, pamoja na kutekeleza diplomasia ya uchumi katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.
“Niwaombe mkawaambie wananchi nini tunafanya kupitia kodi zao ikiwemo pamoja na utekelezaji wa miradi kama ujenzi unaoendelea wa shule mpya za awali na msingi Kata ya Kibirizi na Buhanda, upanuzi wa kiwanja cha ndege Kigoma, ujenzi wa Kituo cha afya unaoendelea Rusimbi, ujenzi unaoendelea wa Barabara ya Bangwe-Ujiji,” amesema Mabuba.
Amesema miradi mingine ni ujenzi unaoendelea wa daraja la Mto Luiche, Shule ya Sekondari ya Mji Mwema, ujenzi unaoendelea wa ukumbi wa kisasa eneo la Mwanga Community Centre, ujenzi unaoendelea wa jengo la utawala.
Ujenzi wa kituo cha afya cha Rusimbi,Manispaa ya Kigoma ujiji kitachawasogezea huduma za afya wananchi wa kata za jirani na wenyeji wa kata ya Rusimbi.
Naye ofisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo, Richard Mtauka amesema kuwa idara ya elimu ya manispaa hiyo imepokea jumla ya Sh2.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule 13 zikiwamo nne mpya.
“Halmashauri yetu ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ina jumla ya shule za msingi 47 na ina jumla ya wanafunzi 51,892 huku tukiwa na upungufu wa madarasa 596 hivyo ujenzi huo wa shule mpya na madarasa utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa miundombinu katika shule zetu za Manispaa,” amesema Mtauka.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya mipango na uratibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Julius Ndele amesema miradi 14 ilitembelewa na waandishi wa habari ni sehemu ya miradi 57, ambapo kiasi cha fedha Sh51.6 Bilioni kimetolewa na Serikali Kuu na Sh2.1 bilioni kutokana na mapato ya ndani.
