ALIYEKUWA mshambuliaji wa Azam FC, Jhonier Blanco amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na timu ya Llaneros ya kwao Colombia, baada ya kutokuwa na timu yoyote tangu alipoachana na wanalambalamba aliowatumikia kwa msimu wa 2024-25.
Baada ya kuondoka Azam, mshambuliaji huyo awali ilielezwa angejiunga na timu ya Independiente Santa Fe ya huko kwao Colombia, lakini dili hilo lilikwama na sasa Llaneros imeingilia kati na kushinda vita hiyo.
Independiente Santa iliyoanzishwa Februari 28, 1941, huko Bogota Colombia, ikiwa inashiriki Ligi ya Categoria Primera A, ilianza mazungumzo mapema na nyota huyo ili kuinasa saini yake, ingawa inaelezwa kuna baadhi ya mambo hawakukubaliana.
Blanco alijiunga na Azam Julai 1, 2024, akitokea Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia, ambapo alisaini mkataba wa miaka minne kukichezea kikosi hicho, lakini alikitumikia kwa msimu mmoja tu wa 2024-2025.
Alipojiunga na Azam, Blanco alikuwa na kiwango cha kupanda na kushuka, ambapo msimu wa 2024-2025, katika Ligi Kuu Bara aliifungia timu hiyo mabao matatu, licha ya mwanzoni kutabiriwa makubwa na mashabiki wa kikosi hicho alipowasili.
Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, alianzia soka lake kwenye akademi ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Aguilas Doradas ambayo ilimtoa kwa mkopo kuichezea Fortaleza CEIF ya Ligi Daraja la kwanza Colombia.
Akiwa na Fortaleza, nyota huyo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza Colombia (Categoria Primera B), baada ya kufunga mabao 13, msimu wa 2022-2023 na kukiwezesha kikosi hicho kupanda daraja, huku kikitwaa pia ubingwa msimu huo.
