Arusha. Urejeshaji wa mandhari ya kimazingira, ulinzi wa vyanzo vya maji, upanuzi wa uhifadhi wa wanyamapori unaoongozwa na jamii, pamoja na uwekezaji katika mifumo ya ikolojia ya kaboni ya buluu (blue carbon), ni miongoni mwa njia zilizotajwa na wadau katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya utalii.
Njia hizo zimetajwa wakati Jukwaa la Wakurugenzi wa Kampuni Tanzania (CEOrt), kwa kushirikiana na Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) na wadau wa sekta ya utalii, kuja na msukumo mpya wa kuhamasisha matumizi ya suluhisho zinazotumia Njia za Asili (NbS) ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika utalii nchini.
Msukumo huo umedhihirika kupitia warsha iliyofanyika jijini Arusha mwishoni mwa wiki, iliyolenga kueneza matumizi ya NbS katika mnyororo mzima wa thamani wa utalii kuanzia uhifadhi wa rasilimali hadi uendeshaji wa biashara kwa lengo la kuimarisha uendelevu na ushindani wa sekta hiyo.
Kikao hicho kiliwakutanisha wataalamu wa uhifadhi, wadau wa sekta binafsi, taasisi za utafiti na wawakilishi wa taasisi za umma wanaosimamia utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya uendelevu na ustahimilivu wa tabianchi.
Warsha hiyo imeratibiwa na wataalamu akiwamo Dk Mike Musgrave wa Kampuni ya New Natural Capital, Dk Gileard Minja na Dk Nyanjige Mayala kutoka Sustainable Tourism Tanzania (STTZ).
Kwa mujibu wa waandaaji, hatua hizo zinaweza kuongeza ushindani wa utalii nchini sambamba na kuboresha viwango vya mazingira, jamii na Utawala Bora (ESG), vinavyozidi kuwa kigezo muhimu kwa wawekezaji na wasafiri wa kimataifa.
Kupitia nguzo yake ya biashara na uendelevu, CEOrt inaendelea kuisukuma sekta binafsi kuwa injini ya mabadiliko ya kijani.
Kupitia Mradi wa Resolve NbS unaofadhiliwa na Norad na kutekelezwa kwa ushirikiano na IUCN, juhudi hizo zinalenga kuwezesha biashara kwa kutoa mwongozo wa vitendo, mifano halisi ya utekelezaji na maarifa ya kifedha ili kujumuisha NbS katika mikakati ya uendelevu na maamuzi ya uwekezaji wa kampuni.
“Utalii ni moja ya sekta zinazotegemea sana mazingira Tanzania,” amesema Meneja wa Miradi wa CEOrt, Hawa Urungu.
“Tukilinda mazingira, tunalinda masoko yetu. NbS zinatoa njia madhubuti kwa waendeshaji utalii kupunguza hatari za tabianchi, kuimarisha ustahimilivu wa vivutio vyetu na kukidhi matarajio ya kimataifa ya uendelevu. Hii si ajenda ya mazingira pekee, bali pia ni ajenda ya ushindani wa kibiashara.”
Aidha katika majadiliano hayo uhifadhi shirikishi, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia ya ukanda wa pwani, kilimo bunifu na endelevu kwa minyororo ya ugavi wa hoteli, pamoja na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira katika maeneo ya utalii ni fursa zilizojadiliwa.
Wadau hao wameserma ujumuishaji wa NbS unaweza kuboresha uzoefu wa watalii, kulinda urithi wa Taifa na kufungua vyanzo vipya vya uwekezaji wa kijani, hasa katika kipindi ambacho wasafiri wengi wa kimataifa wanapendelea maeneo yenye athari chanya kwa mazingira.
Hata hivyo, licha ya hatua zilizopigwa, wamesisitiza haja ya kuimarishwa kwa msaada wa kitaalamu, upatikanaji wa fedha mahsusi na sera wezeshi.
Baadhi ya kampuni za utalii zilionesha nia ya kupanua miradi ya NbS lakini zikatolea mfano changamoto za gharama za awali, ukosefu wa motisha na uratibu hafifu wa taasisi kama vikwazo vinavyokwamisha kasi ya utekelezaji.
