Chama la kina Lunyamila linakwama hapa

CHAMA la Watanzania wawili, Julietha Singano na Enekia Kasonga ‘Lunyamila’ wanaokipiga FC Juarez inayoshiriki Ligi ya Wanawake Mexico bado lina changamoto kwenye eneo la ushambuliaji.

FC Juarez iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 18, kwenye mechi 17 imeshinda saba, sare sita na kupoteza nne ikifunga mabao 24 na kuruhusu 27.

Ikumbukwe timu hiyo msimu uliopita haikuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao ilitikisa nyavu za wapinzani mara 21 ikiwa ni idadi ndogo ya mabao hasa kwa washambuliaji ikamsajili Opah Clement kwa sasa anaitumikia SD Eibar ili kutibu tatizo kwenye eneo la ushambuliaji naye akacheza mechi sita kati ya 17 bila bao wala asisti.

Timu hiyo ikaingia tena sokoni na kumsajili mtanzania mwingine Lunyamila ambaye alikuwa na msimu bora akiwa na Mazaltan ya nchini huko alipofunga mabao sita kwenye msimu wake wa kwanza.

Kwa sasa timu hiyo inamtegemea Lunyamila katika eneo la ushambuliaji lakini hadi sasa amecheza mechi 15 akifunga bao moja na asisti tatu.

Ukiachana na Lunyamila hata washambuliaji wengine hawana rekodi nzuri ya kufunga, anayeongoza kwa ufungaji ni kiungo Jasmine Alexis mwenye mabao sita.

Ikiwa raundi ya kwanza ya ligi hiyo imetamatika zikiwa zimechezwa mechi 17 mshambuliaji pekee mwenye bao hadi sasa ni Lunyamila ambaye ana moja, huku viungo wakitawala kwenye upachikaji wa mabao.