Dar es Salaam. Katika pitapita zangu huku mitaani, kila karibu kila mzazi ninayekutana naye na kufanya naye mazungumzo hususan wale wenye watoto wanaosoma na wanaotarajia kuanza shule, mazungumzo yao ni jinsi wanavyohangaika kupata shule nzuri kwa ajili ya watoto wao.
Nikawa najaribu kurudisha nyuma enzi mimi nasoma na ndugu zangu, namna wazazi wangu walivyokuwa wanahangaika kuona tunapata shule bora.
Ndipo nilipojifunza kuwa kumtafutia mtoto shule nzuri si suala la bahati nasibu, bali ni mchakato unaohitaji umakini, utafiti na uamuzi sahihi.
Nakumbuka baba yangu alichokuwa akikifanya kwanza ni kutuelewa sisi watoto wake tunapenda kitu gani, pili alikuwa anachunguza falsafa ya shule kwa kuzingatia ubora wa walimu, kuangalia mazingira, kutathmini kazi za ziada wanazopewa wanafunzi shuleni, lakini pia alikuwa akizungumza na wazazi wenye watoto kwenye shule hizo, akilenga kujifunza zaidi kuhusu shule husika.
Nilipofika kidato cha nne, nilikuja kubaini kwamba baba alikuwa akifanya vile, kwa lengo la kupata shule sahihi ambayo ingetujenga vema kitaaluma, lakini pia kimalezi.
Kwani Waswahili husema shule njema humjenga na kumuandaa vema mtoto aje kuwa raia mwajibikaji na mwenye mafanikio katika maisha yake ya baadaye.
Tukumbuke katika jamii yoyote, elimu ndiyo ufunguo wa maisha yenye mafanikio. Kwa mzazi au mlezi, jukumu la kumtafutia mtoto shule bora ni miongoni mwa uamuzi mzito na wenye athari ziwe chanya au hasi za muda mrefu.
Wakati mwingine, wazazi hujikuta wakisumbuliwa na maswali mengi; ni shule ipi inaweza kumjenga mwanawe vizuri, Je! mazingira yake ni salama? Au gharama zake zinaendana na huduma?
Wataalamu wa elimu wanasisitiza kuwa hatua ya kwanza katika kuchagua shule ni kumwelewa mtoto mwenyewe.
Watoto hutofautiana katika uwezo, utu, kasi ya kujifunza na mahitaji ya kiakili. Kwa kutambua tofauti hizi mapema, mzazi anaweza kupata mwelekeo mzuri kuhusu aina ya mazingira yanayomfaa mtoto wake.
Ikiwa mtoto ni mwenye aibu, anahitaji shule yenye walimu wanaoweza kumtia moyo; ikiwa ana uwezo mkubwa wa ubunifu, anahitaji shule yenye nafasi za kubuni na kuchunguza.
Kwa sababu tunaambiwa kuwa falsafa na mfumo wa ufundishaji mara nyingi ndiyo huwa msingi mzuri wa mafanikio.
Mara zote wazazi wanapaswa kuelewa kwamba shule hazifanani katika mitazamo na mbinu za ufundishaji. Baadhi hutumia mtalaa wa kitaifa, nyingine mifumo shirikishi au mtalaa wa kimataifa. Ni jukumu la mzazi kuchunguza, kuuliza na kufahamu kwa undani mfumo unaotumiwa na shule anayolenga kumpeleka mwanawe.
Niliwahi kuambiwa na mtaalamu mmoja wa elimu kwamba, mfumo bora ni ule unaomuweka mwanafunzi katikati ya mchakato wa kujifunza, unaomjenga kufikiri kwa uhuru, kutatua matatizo na kujiamini katika kuwasiliana.
Hivyo, walimu na uongozi ni nguzo muhimu ya ufanisi kwa wanafunzi. Nasema hivyo kwa sababu ubora wa elimu hauwezi kutenganishwa na ubora wa walimu.
Mwalimu mwenye mafunzo ya kutosha na ujuzi wa kuwahudumia watoto, hutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma na kimalezi.
Kwa maana hiyo, mzazi anashauriwa kuuliza kuhusu kiwango cha elimu cha walimu, uzoefu wao na kama shule inatoa mafunzo endelevu ili kuwajengea uwezo.
Vilevile, uongozi wa shule unapaswa kuwa wenye maono na unaothamini ushirikiano kati ya shule na wazazi. Mara zote uongozi dhaifu mara nyingi huishusha hadhi ya shule na huathiri maendeleo ya watoto.
Tukumbuke kwamba kwa mtoto, shule ni kama nyumba yake ya pili. Hivyo, mazingira yake yanapaswa kuwa salama, safi na rafiki kwa ujifunzaji. Mzazi anapaswa kutembelea shule tarajiwa ya mwanawe ili kujionea hali ya madarasa na mazingira ya kujifunzia kwa ujumla kabla ya kufanya uamuzi.
Shule yenye mazingira duni kwa kawaida huathiri na kupunguza ari ya mtoti kujifunza.
Maendeleo ya mtoto hayaishii darasani. Michezo, sanaa, muziki, kilimo na klabu za ubunifu ni maeneo muhimu yanayojenga utu na uwezo wa mtoto.
Shule bora huweka uwiano mzuri kati ya masomo ya darasani na shughuli hizi zinazotengeneza watoto wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kushirikiana, kuongoza na kutatua matatizo.
Moja ya vyanzo bora vya kupata taarifa sahihi kuhusu shule, ni wazazi ambao watoto wao tayari wanasoma hapo. Maoni yao yanaweza kuweka wazi mambo ambayo hayataonekana katika vipeperushi au taarifa rasmi za shule.
Kupitia wao, mzazi anaweza kupata picha ya jinsi shule inavyoshughulikia nidhamu, mawasiliano na wazazi, na maendeleo ya wanafunzi. Ushahidi wa jamii mara nyingi huonyesha uhalisia wa utendaji wa shule.
Ingawa ada kubwa si kipimo cha ubora, ni muhimu kuhakikisha kuwa gharama za shule zinaendana na huduma na mazingira yanayotolewa. Mzazi anaweza kulinganisha shule kadhaa ili kupata thamani bora kulingana na uwezo wake kifedha.
Lengo si kupata shule ya gharama kubwa, bali shule inayotoa ubora wa elimu unaostahili kwa kiwango cha ada kinacholipwa
