Israel yadai kumuua kamanda mwandamizi wa Hamas Gaza

Jeshi la Israel limesema limemuua kamanda mkuu wa Hamas katika shambulio lililolenga gari lililokuwa likipita kwenye Jiji la Gaza siku ya Jumamosi.

katika taarifa ya pamoja ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) na Shirika la Usalama la Shin Bet walieleza kuwa Raed Saad, aliyekuwa mkuu wa uzalishaji wa silaha wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Qassam, ameuawa katika operesheni hiyo.

Saad alitajwa kuwa miongoni mwa makamanda mashuhuri wa Brigedi za Qassam na alihusika kuongoza brigedi kadhaa wakati wa mashambulizi ya Hamas dhidi ya jamii za Israel mashariki mwa Jiji la Gaza mwanzoni mwa vita.

Msemaji wa ulinzi wa raia anayeongozwa na Hamas, Mahmoud Basal, aliliambia Shirika la habari la BBC kuwa watu wanne waliuawa katika shambulio hilo, huku wapita njia wengi wakijeruhiwa kutokana na mlipuko.

Ofisa wa Hamas katika eneo la Gaza pia aliiambia BBC kuwa shambulio hilo lilimuua msaidizi wa Saad pamoja na ofisa mwingine wa cheo cha chini anayefahamika kwa jina la abu Imad al Laban.

Taarifa ya IDF na Shin Bet iliongeza kuwa Saad alihusishwa na vifo vya wanajeshi wengi wa Israel waliouawa ukanda wa Gaza kutokana na matumizi ya vifaa vya kulipuka.

kwa mujibu wa taarifa hizo, Saad alikuwa anaaminika kuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza jipya la uongozi wa kijeshi la Hamas lenye wajumbe wachache, lililoanzishwa baada ya kuanza kwa harakati za kusitishwa mapigano Oktoba mwaka huu.