BAADA ya kukubali kichapo cha mabao 6-0 kutoka kwa JKT Queens, kocha wa Bilo Queens, Ibrahim Humba, amesema ugeni wa Ligi Kuu na uzoefu mdogo wa mashindano ni kati ya sababu zilizowaangusha.
Bilo Queens ni kati ya timu nne zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza, ikiuwakilisha Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Humba amesema walijikuta wakiingia kwenye mfumo wa wapinzani wao, hali iliyowafanya washindwe kudhibiti mchezo huku JKT Queens wakionekana kuwa bora katika kila eneo kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji. “Tulianza mchezo vizuri lakini kadri dakika zilivyoenda tukawa tunashambuliwa sana. JKT Queens walikuwa na kasi na walitumia vyema nafasi walizopata tukashindwa kujiamini,” amesema Humba.
Aliongeza kuwa presha ya kucheza ligi ya juu kwa mara ya kwanza ilichangia makosa ya mara kwa mara, hasa katika safu ya ulinzi, hali iliyowapa wapinzani nafasi ya kuongeza mabao.
“Hii ni ligi tofauti kabisa na Daraja la Kwanza. Makosa madogo yanakuadhibu haraka. Tulijifunza kwa uchungu, lakini ni somo kubwa kwetu kama timu mpya.”
Kocha huyo amesema licha ya kipigo hicho kikubwa, bado ana imani na kikosi chake, akibainisha kuwa watafanya marekebisho ya haraka kwa mechi zijazo.
“Tutakaa chini kurekebisha makosa, kuongeza nidhamu ya ulinzi na kuwajenga kisaikolojia wachezaji. Lengo ni kubaki ligi kuu.”
Katika hatua nyingine timu ya Alliance Queens yenye maskani jijini Mwanza imeanza vyema kuchanga karata katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo wakiwa nyumbani Nyamagana, lakini kuna rekodi mbovu imeivunja ya miaka minne.
Timu hiyo ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ceasiaa Queens ya Iringa kisha ikafanya hivyo tena dhidi ya Fountain Gate ikaichapa bao 1-0.
Rekodi yenyewe ni kwamba Alliance na Fountain Gate zilikutana mechi tisa na mara ya mwisho Wanamwanza hao kupata ushindi ilikuwa mwaka 2021 kwani mechi nyingine zote ilikuwa ikiambulia vipigo tu.
Mechi ya kwanza kukutana mwaka huo Alliance ilishinda mabao 3-2 baada ya hapo Fountain waliboresha timu hiyo na hawakukubali tena kichapo.
Kati ya mechi tisa Alliance imeshinda mbili, sare moja na kupoteza sita.
Tangu hapo ni kama imepita miaka minne sasa Alliance iliyojaa wachezaji wachanga ikiwa chini ya kocha Sultan Juma imevunja mwiko huo juzi.
