Mabula atamani rekodi mpya Azerbaijan

KIUNGO wa Shamakhi FC inayoshiriki Ligi Kuu Azerbaijan, Alphonce Mabula amesema anatamani kuvunja rekodi yake binafsi ya msimu uliopita baada ya kufikisha mabao matatu na asisti tatu alizochangia 2024-25.

Huu ni msimu wa pili wa kiungo huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars kuitumikia timu hiyo. Msimu uliopita alicheza nusu msimu alipojiunga na Shamakhi akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia alikocheza kwa misimu miwili.

Mabula amesema msimu uliopita alifunga mabao matatu na kutoa asisti tatu, lakini msimu huu anaamini anaweza kufanya zaidi kutokana na uzoefu alioupata pamoja na maandalizi bora aliyoyafanya.

“Msimu uliopita ulikuwa wa kujifunza, lakini sasa nina uzoefu zaidi na naamini kabisa ninaweza kuvunja ile rekodi. Malengo yangu ni kusaidia timu kwa mabao na asisti nyingi zaidi,” amesema Mabula.

Kiungo huyo aliongeza kuwa kujiamini kwake kumechangiwa na mwendelezo mzuri wa mazoezi pamoja na imani kutoka kwa benchi la ufundi, jambo linalompa motisha ya kupambana.

Wakati huohuo, Mabula alithibitisha kuwa jana alianza safari ya kujiunga na kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, iliyopo Misri, ambako kikosi hicho kinajiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Ni heshima kubwa kuitwa timu ya taifa. Naenda kambini nikiwa na malengo ya kufanya kazi kwa bidii na kujifunza zaidi.”