Mafuriko Gaza yaua watoto watatu, maelfu waachwa bila makazi

Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa pamoja na uharibifu wa miundombinu katika ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya watoto na kuongezeka kwa mateso ya wakazi waliokwishaathiriwa na vita, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa.

Kwa mujibu wa shirika la ulinzi wa raia Gaza, watoto watatu wamefariki dunia baada ya maji kuvamia mahema na makazi ya muda, huku wawili wakifariki katika Jiji la Gaza na mmoja katika eneo la Khan Yunis. Taarifa hiyo imethibitishwa pia na Hospitali ya Al Shifa iliyoeleza kuwa miongoni mwa watoto waliofariki ni msichana wa miaka tisa, Hadeel al Masri, pamoja na mtoto mchanga, Taim al Khawaja, wote kutoka katika Jiji la Gaza.

Mtoto wa miezi minane, Rahaf abu Jazar, alifariki eneo la Khan Yunis baada ya maji ya mvua kuvamia kwenye hema la familia yake na kusababisha baridi kali.

BBC News imeripoti kuwa mvua hizo zimeathiri zaidi maeneo ya kaskazini na kati ya Gaza, ambako familia nyingi zimekimbilia baada ya makazi yao kuharibiwa na mashambulizi ya kijeshi, huku maji yakivamia mahema na kusababisha vifo na majeruhi.

Kwa upande wake, Al Jazeera imesema mafuriko hayo yameathiri zaidi kambi za wakimbizi, ambapo watoto wachanga wanakabiliwa na baridi kali, magonjwa na uhaba wa huduma za afya, hali inayoongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.

Reuters imenukuu mashirika ya misaada yakieleza kuwa uharibifu wa mifumo ya maji taka, barabara na umeme umeifanya hali kuwa mbaya zaidi, na kuwaacha maelfu ya watu bila makazi salama wala huduma za msingi.

Akizungumza na vyombo vya habari, msemaji wa ulinzi wa raia anayeongozwa na Hamas, Mahmoud Basal, amesema mafuriko hayo ni tishio jipya kwa maisha ya raia, hasa watoto, huku mashirika ya kibinadamu yakitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufungua njia za misaada na kutoa msaada wa haraka kabla hali haijazidi kuwa mbaya.

Wakazi wa Gaza wamesema mafuriko hayo yameongeza mateso juu ya maumivu ya vita vinavyoendelea, wakihofia idadi ya vifo kuongezeka endapo msaada wa dharura hautapatikana kwa wakati.