Mbarali kutenga Sh1 bilioni kuboresha maeneo korofi

Mbarali. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, inatarajia kutumia zaidi ya Sh1 bilioni kwa ajili ya kuboresha maeneo korofi ya miundombinu barabara za  pembezoni .

Katika hatua nyingine imeweka mikakati ya kutenga bajeti ya mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha kwa lengo la kununua mtambo wa kisasa wa kuchonga na kuboresha miundombinu ya barabara.

Hatua hiyo imeelezwa kuhakikisha maeneo muhimu ya sekta ya elimu na kilimo yanafikika ili  kuepuka madhara yatokanayo na athari za msimu wa  mvua nyingi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond  Mweli  amesema leo Jumapili Desemba 14,2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital  kuhusiana na miradi mbalimbali wanayo tekeleza kupitia mapato ya ndani.

“Tumejipanga kikamilifu kutekeleza miradi mbalimbali  ya kimkakati kwa  kutumia mapato ya ndani kwenye  sekta ya elimu, afya, kilimo, barabara na maji  lengo ni kuona tunafikia mipango  tuliojiwekea kufikisha huduma kwa wananchi,” amesema.

Mweli amesema kimsingi asilimia 80 ya mapato ya halmashauri inategemea sekta ya kilimo ambapo kwa kipindi cha mwaka  2024/2025, walikusanya  Sh10 bilioni na mwaka 2025/2026 malengo ni kukusanya Sh12 bilioni.

“Tumeweka mikakati ya kusaka vyanzo mbalimbali vya mapato ili kufikia kukusanya Sh12 bilioni, lakini kuboresha miundombinu ya kilimo na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima na  ujenzi wa mradi wa  skimu 100  za umwagiliaji,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha sekta ya kilimo inaboreshwa tayari wamepokea matrekta madogo  76, kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia Wizara ya Kilimo ambayo yataleta tija ya kuongeza uzalishaji.

“Matrekta hayo yatatolewa kwa wakulima wa zao la mpunga, lakini tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo kubwa kuwekeza nguvu kwenye sekta ya kilimo iliyo na mchango mkubwa kwa pato la Taifa,” amesema.

Mweli amesema zaidi ya migogoro ya ardhi 100 wamepokea ambayo iko katika hatua mbalimbali za utatuzi sambamba na kuanza kurasimisha maeneo na kutoa hati kwa wananchi ili kuondokana na changamoto hiyo.

“Mpaka sasa tayari tumerasimisha maeneo  mbalimbali na kutoa hati 14 kwenye taasisi za elimu ili kuepuka changamoto  za migogoro ya ardhi inayokwamisha jitihada za Serikali,” amesema.

Mweli ameonya baadhi ya watumishi wa Serikali kutokuwa  chanzo cha kuchochea migogoro ya ardhi kwa  wananchi wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Mkulima wa zao la mpunga kutoka Kata ya Kapunga, Ester  Amos amesema utaratibu wa Serikali kuboresha miundombinu utawasaidia kufikisha zao la mpunga sokoni kwa wakati na kudhibiti walanguzi.

Naye Solomon Oscar, Mkazi wa Madibira wilayani humo, amesema wanaomba mkakati huo  wa halmashauri kuboresha miundombinu ufanyike kwa haraka kabla ya mvua za msimu hazijachanganya.