Miaka saba ya visa na mikasa ya dalali kuvusha wanafunzi Tegeta

Dar es Salaam. “Nilishuhudia ajali za mara kwa mara nikaamua kujipa jukumu hili,” ni kauli ya Salum Seif akielezea miaka saba ya msaada wake kwa watoto na watu wengine kuwasaidia kuvuka barabara katika eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam.

Eneo hilo liliripotiwa kuwa na ajali za mara kwa mara hasa kwa wanafunzi waliokuwa wakivuka kwenda Shule za Msingi Pius Msekwa na Kunduchi zilizopo Wilaya ya Kinondoni kutokana na mwendo kasi wa vyombo vya moto katika barabara ya Bagamoyo.

Akizungumza na Mwananchi Seif ambaye pia dalali anasema kutokana na ushuhuda wa ajali zilizokuwa zinatokea mara kwa mara, aliamua kuchukua jukumu la kuwavusha watoto wanapokwenda shule na kurudi kuanzia saa 11 alfajiri hadi 12 jioni tangu mwaka 2018.

“Niliamua kufanya kazi hii baada ya kuona watoto wanagongwa katika eneo hili, nikajiuliza kwa nini nikimbilie kuangalia watoto walivyoumizwa au kufa wakati ninauwezo wa kuwasaidia nikaamua kuifanya kazi hii kwa upendo mkubwa,” anasema Salum.

Licha ya kazi yake ya kujitolea, sio kila mtu anayeshukuru, anasema baadhi ya wenye magari wamekuwa wakimlalamikia kwa kile wanachokiita kupoteza muda wanaposimama kuwapisha watoto kupita.

Anasema pamoja na chuki hizo, haikumfanya aache shughuli hiyo kwa sababu ameamua kujitolea kwa watoto na si kitu kingine kwa kuamini kesho ya watoto anaowavusha.

“Wanachukia lakini siwavushi watoto pekee hata watu wazima nawasaidia japokuwa malengo yangu yapo kwa watoto zaidi na nafanya kazi hii kwa siku nzima,” anasema.

Anasema kazi yake haina likizo hata wanafunzi wasipokuwepo anaendelea na kazi ya kuvusha watu wanaotumia barabara hiyo wakati wote bila kujali suala la masilahi.

Salum anasema mbali na kazi ya kuvusha watoto pia ni dalali wa nyumba na vyumba vya biashara, hivyo anapopata mteja kuna watu anawaachia kwa ajili ya kusaidia kuvusha watoto wanapotoka shule.

“Hii kazi sasa si ya peke yangu tu, wakati mwingine nikiondoka kufanya kazi yangu ya udalali nawaachia wengine kusaidia wakiwamo bodaboda kuvusha watoto wanaokuwa wanatoka shule,” anasema.

Anasema polisi wa vyombo vya usalama barabarani wameona juhudi zake na kuamua kumsaidia kwa njia wanazoweza na mara kadhaa wameweka doria eneo hilo, kuhakikisha magari yanaheshimu juhudi zake.

“Kwa kutambua umuhimu wangu hata aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro alikuwa anasimama na kunisalimia hapa kila atakapopita hata alipotolewa na kupewa mtu mwingine nafasi alikuwa anapita na kunisalimia siku moja moja,” anasema.

Anasema inapotokea msafara, askari wa barabarani huwa wanamwambia na wao wakiwa katika eneo hili kuhakikisha taratibu zilizowekwa zinafuatwa.

Anasema wakati akiendelea na kazi hiyo ya kujitolea mwaka 2021 alipata ajali ya kugongwa na pikipiki wakati anavusha watoto na kuvunjika mguu.

“Ajali niliyopata sikuitegemea kwa sababu nilikuwa naangalia upande yanapotokea magari na sikuwa na wasiwasi kuhisi kama kuna pikipiki itatokea upande mwingine ghafla akanigonga nikapelekwa Muhimbili,” anasema.

Anasema akiwa hospitalini hapo, wanafunzi na walimu wa shule za Pius Msekwa na Kunduchi walimchangia Sh300,000 kwa sababu ya kutambua umuhimu wake katika kuvusha watoto.

Anasema kiasi hicho cha pesa kilisaidia kupata huduma, alihitaji kuwekewa chuma mguuni na kufanikiwa na aliporejea mtaani aliendelea na kazi hiyo huku wanaotambua mchango wake wamekuwa wakimpa shukrani.

“Mbali na hao yupo mtu ambaye huwa ananipa Sh10,000 akipita hapo japokuwa sio kila siku inaweza kupita hata mwezi kwa kuwa anajitolea haoni kama kuna tatizo kutokupata pesa,” anasema.

Pia, anasema kutokana na ajali hiyo, huwa yanaibuka maumivu kwenye mguu ulioumia, ambayo humfanya kwenda Hospitali ya Kitengule kwa ajili ya uchunguzi.

“Sipo kazini leo kwa sababu ya maumivu ya mguu na nilikwenda Hospitali ya Kitengule kujua nini tatizo, hata hivyo wameniambia nirudi tena kesho (Ijumaa),” anasema Salum.

Juhudi za Salum hatimaye ziligusa mioyo ya wahandisi wa mradi wa barabara ya mwendokasi inayopita eneo hilo, baada ya kushuhudia kazi yake, waliamua kuweka alama ya pundamilia kwenye sehemu hiyo.

“Wajenzi wa barabara waliona tunavyopata tabu wakaamua kuweka alama ya kivuko na kutupatia kiakisi mwanga, lakini bado madereva hawazingatii hili na kuona si la muhimu,” anasema.

Anasema alikuwa ana mke na mtoto mmoja lakini hivi sasa yupo mwenyewe baada ya kuachana na mkewe na mtoto wake kufariki dunia na hiyo imekuwa ikimzidishia zaidi upendo kwa watoto.

“Sioni shida kufanya hii kazi na hakuna mtu anayeweza kunikataza nisifanye kwa sababu nipo mwenyewe sina familia kwa sasa na ndugu zangu hawawezi kusema chochote kwa sababu ni maisha niliyochagua,” anasema.

Msaidizi wake Anania Masumbuko anasema tangu wameanza kufanya shughuli hiyo ya kuvusha watoto ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa na wakati mwingi inaweza kupita hata mwaka hakuna mtoto aliyegongwa.

“Jambo tunalolifanya limekuwa na faida kwakuwa imefika hatua wazazi wanabaki nyumbani na kuwaruhusu watoto wao waende shule wenyewe wakiamini kuna usalama barabarani,” anasema Masumbuko.

Anasema watoto wakifika barabarani wanawaita kwa ajili ya kuvushwa hata kama wakiwepo upande mwingine wa barabara kwa kuwa ni watu pekee wanaowaamini.

“Kama tutakuwa tumepumzika watoto wanaita babu au bodaboda wanasaidia kuita na kusema njooni mchukue watoto wenu huku kwa kuwa tumejitolea kufanya hiyo kazi, hatuna budi kwenda kuwachukua na kuwavusha,” anasema.

“Ningependa kuona Serikali ikiweka madaraja ya kuvukia kwa watoto wetu. Hii kazi ninayofanya ni kwa sasa, lakini tunahitaji suluhisho la kudumu,” anasema.

Masumbuko anasema changamoto iliyopo ni madereva kutokutii sheria za barabarani kusimama kwenye alama ya pundamilia hata wanaposimamishwa, hivyo kuamua kutumia nguvu kwa ajili ya kutii.

“Baada ya kuona madereva hawataki kusimama hususani bodaboda tumeamua kuwa na fimbo za kuwapiga pale wanapopita wakati wa watu wanavuka barabara, hii imekuwa kero sana,”anasema.

Anasema wapo madereva ambao wamekuwa na ujeuri hata kama watu wameshaingia kwenye kivuko ‘zebra’ husasani magari ya Serikali, huwa hawasimami inapotokea wamesimaishwa ili kuruhusu watu wavuke.

Mbali na hilo, anasema wamejikuta kwenye wakati mgumu inapotokea ajali kwa kuwa, wazazi wa mtoto husika hutokea hospitali kwa kuchelewa na kukuta mtoto ameshahudumiwa.

“Inaweza kutokea ajali asubuhi tukahangaika na mtoto kuanzia polisi hadi hospitali lakini mzazi anajitokeza mchana na sisi hatuwezi kumuacha mtoto mwenyewe hospitali bila uangalizi,”anasema Masumbuko.

Dereva wa daladala za Tegeta, Sebastian Nyoni anasema analolifanya Salum ni zuri kwa kuwa, limesaidia kupunguza ajali kwa wanafunzi wanaokwenda na kutoka shule kutokana na ukubwa wa barabara hiyo.

“Nawasifu kwenye hili, tunajua ni jukumu la polisi kuwepo eneo hili lakini kuna watu wamejitolea kufanya hivyo kwa ajili ya kuwasaidia na huu ndiyo uzalendo,”anasema Nyoni.

Akizungumza na Mwananchi Desemba 5, 2025, Mkaguzi wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Dumu Mwalugenge anasema katika udhibiti wa ajali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine wamejikita katika kufanya operesheni za kudhibiti makosa hatarishi.

“Operesheni hizi ni endelevu na zinaenda sambamba na utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote yanayotumia barabara, huku hadi shuleni kufundisha alama za matumizi ya taa” anasema Mwalugenge.

Anasema makundi hayo ni pamoja na madereva, wapanda pikipiki, watembea kwa miguu, wapanda baiskeli, wasukuma mikokoteni, waendesha maguta, wanafunzi, watu wenye mahitaji maalumu na abiria katika magari.

Pia, anasema madereva wa Serikali wanapaswa kufuata sheria na kuwa mfano wa kuigwa kwasababu wameuwa wakilalamikiwa kwa kuvunja sheria na hawatasita kuwachukulia hatua za kisheria.