Mwabudu Mungu aliyethibitika upate kuwa na amani maishani

Dar es Salaam. Bwana Yesu asifiwe. Karibu katika somo la mahubiri leo Jumapili. Hili ni somo litakalokufanya usimame vyema katika kumwabudu huyu Mungu wa kweli, anayesema, “Mimi Niko ambaye Niko” Yehova ndilo jina lake.

 Ninaitwa Hosea Gambo, mtumishi wa huyu Mungu ninapatikana Kanisa la HRCC TAG Haydom, Mbulu mkoani Manyara.

1 Fal 18:36-37 “Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.

“ …Nabii wa Mungu, Eliya katika kipindi cha utawala wa Ahabu mfalme wa Israel, alibaki nabii pekee wa Mungu na walikuwepo takriban manabii 450 wa miungu baali. Eliya alitaka ithibitike kwamba Mungu wa kweli anayestahili kuabudiwa ni Mungu yupi.

Biblia inasema, 1 Fal 18:21 “Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.” …watu walikuwa wamechanganyikiwa na hawakuwa wamekaa pasipo kuwa na ibada ya kweli.

Ninaweza kusema watu wa Israel wa kipindi hicho ni sawa na watu katika dunia ya leo. Watu katika ulimwengu wa sasa hawajui waende wapi, wamebaki njia panda; mara wakibanwa na changamoto na majaribu wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji au wanakwenda kwa mashekhe; mara wanaenda kwa wachungaji mara kwa mapadri. Hawana uhakika ni Mungu yupi wamnyookee na anayestahili.

Ninataka leo hii ijulikane ni kwanini unapaswa kumwabudu huyu Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Yakobo; huyu anayethibitishwa na nabii Eliya. Huyu Mungu amethibitika, manabii 450 wa mungu baali walimshuhudia ana kwa ana kuwa ndiye Mungu wa kweli.

Nipende kushirikisha ushuhuda wa kiwete aliyetelekezwa na wanaume wawili wenye nguvu kwenye majanga ya mafuriko ya matope (maanguko ya udongo) kutoka mlima Hanang’ Kateshi; aliachwa katikati ya bonde ambalo liliendewa kwa kasi na mafuriko ya matope. Wale wanaume waliokuwa wanamsaidia siku zote walipoona hali ya hatari wakaanza kujiokoa, wakamwacha hali hawezi hata kujisogeza. Kiwete alimlilia Mungu, “Ee Mungu ninaowategemea wameniacha sijiwezi, sina la kufanya, ninaomba wewe pekee uniokoe” …Huyu kiwete yupo hai na wale wanaume wawili wamekufa katika janga hilo. Huyu Mungu anathibitika hata sasa na ndiye Mungu anayestahili kuabudiwa.

Kwa matendo ya Mungu mbele ya Eliya nabii wa Mungu na manabii 450 wa baali, pamoja na kundi kubwa la wana wa Israel; ndipo watu wote wakafikia uamuzi baada ya kuthibitika Mungu wa kweli… Biblia inasema, 1 Fal 18:39, “Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu.” …Baada ya siku hiyo, watu wote wakamwabudu Mungu wa kweli. Na hata wale wa mbali wanaoabudu miungu yao, walipopata habari hizi walijua yakwamba, wanaabudu matope bali wanapaswa kumwabudu Mungu aliyethibitishwa na Eliya mbele ya manabii wa mungu baali.

Yalimkuta na Nebukadreza Mkuu, Mfalme wa dola kuu ya Babeli. Biblia inasema, Dan 3:28, “Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie miungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.” Sote tunafahamu habari hizi za Mungu kuwaokoa Shadraka, Meshaki na Abednego kwenye tanuri la moto baada ya kukataa kumwabudu mungu wa Mfalme Nebukadreza ile dhahabu iliyosimamishwa mbele ya watu ili iabudiwe. Mungu wa kweli alithibitika.

Nebukadreza mwenyewe akiwa mbele za watu mbele ya yule mungu wa dhahabu aliyesimamishwa naye, watu wakiwa wamesujudia kwa yule mungu; anapaza sauti yake mfalme na kuwaambia ya kuwa ahimidiwe huyu Mungu aliyethibitika.

Mungu wa kweli anajithibitisha mwenyewe na hata sasa anathibitika …kama maandiko yanavyosema ndivyo anavyofanya tangu zamani hata sasa. Mungu huyu ni yule yule tangu kale hata sasa hata wakati ujao.

Nakusihi msomaji wa ujumbe huu, mgeukia Mungu aliyethibitika na kumwabudu, pekee ndiye anayestahili kuabudiwa.  Ngoja nikwambie kitu, watu wagumu kama akina Farao, kina Nebukadreza na ufahari waliokuwa nao walijisalimisha kwa huyu Mungu;

Ushauri na maombezi mawasiliano 0766574220/0788574220.