MABOSI wa TRA United zamani Tabora United, wanaangalia uwezekano wa kumpata kwa mkopo nyota wa Yanga, Denis Nkane, baada ya mchezaji huyo anayecheza nafasi mbalimbali uwanjani kushindwa kupenya kikosi cha kwanza kutokana na ushindani uliopo.
Hatua ya uongozi wa TRA United kuanza msako huo wa kuiwinda saini ya Nkane, unaanza baada aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Mwanengo kudaiwa ameshasaini Yanga hivyo, muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa ndani ya kikosi hicho.
Kiongozi mmoja wa TRA United, aliliambia Mwanaspoti ni kweli mazungumzo ya kuipata saini ya nyota huyo yapo, japo suala nzima la usajili wake litaamuliwa na benchi la ufundi la kikosi hicho, chini ya kocha mkuu, Mrundi Etienne Ndayiragije.
“Ni mchezaji tunayeamini anaweza kuongeza kitu kikubwa kwetu kwa sababu ana uzoefu wa kutosha, ila kama nilivyosema pia hapo mwanzoni sisi tunasubiria kauli ya benchi la ufundi kabla ya kufanya uamuzi wetu wa mwisho,” amesema.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa kati ya makubaliano waliyoingia na Etienne aliyejiunga na timu hiyo akitokea Police aliyoipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2024-2025, ni pamoja na kumpa uhuru wa kufanya usajili kwa nyota atakaowahitaji.
“Baada ya kufanya mazungumzo ya kumuhitaji alitupa vipaumbele vyake na sisi tulimpa vya kwetu, kati ya mambo aliyosisitiza ni kumpa uhuru katika usajili hasa huu wa dirisha dogo, jambo ambalo sio shida kwa sababu tunamuamini.”
Nkane anayeweza kucheza beki wa kulia, winga na kiungo mshambuliaji, alijiunga na Yanga Januari Mosi 2022, akitokea Biashara United.