Dar es Salaam. Ongezeko la watu Tanzania limetajwa kuwa sababu ya kuongezeka kwa kwa uzalishaji bia na vinywaji baridi katika viwanda vya nchini kwa miaka mitano mfululizo.
Bidhaa hizo mbili pia ndiyo zilizozalishwa kwa wingi na viwanda vya ndani katika mwaka 2024 kuliko bidhaa nyingine zilizotajwa kwa upande wa Tanzania Bara.
Ripoti ya Statistical Abstract ya mwaka 2024 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2024 inaonesha uzalishaji bia uliongezeka kwa asilimia 67.5 kati ya mwaka 2020 hadi 2024 huku vinywaji baridi vikiongezeka kwa asilimia 85.2.
Hiyo ina maana kuwa, lita milioni 385.85 zilizalishwa mwaka 2020 kiwango kilichoongezeka hadi kufikia lita milioni 646.5 mwaka 2024 huku uzalishaji wa vinywaji baridi ukiongezeka kutoka lita milioni 839.07 hadi lita 1.55 bilioni mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa za hali ya uchumi wa kikanda ya robo mwaka iliyoishia Desemba 2025 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaitaja Dar es Salaam kuongoza kwa mapato yatokanayo na bidhaa hizo.
Katika robo ya Desemba mwaka jana, mauzo ya bia yalifikia Sh592.9 bilioni kutoka Sh111.8 kipindi kama hicho mwaka uliotangulia huku vinywaji baridi mauzo yakifikia Sh190.7 bilioni kutoka Sh152 bilioni mtawaliwa.
Mauzo ya bia Kanda ya Ziwa, Desemba mwaka jana yalifikia Sh110.4 bilioni kutoka Sh98.6 mwaka uliotangulia huku vinywaji baridi mauzo yake yakishuka hadi kufikia Sh83.4 kutoka Sh90.1 bilioni.
Nyanda za Juu Kusini mauzo ya bia yalifikia Sh47.5 bilioni kutoka Sh42.3 bilioni huku mauzo ya vinywaji baridi yakishuka hadi kufikia Sh40.5 kutoka Sh63 bilioni mtawaliwa.
“Dar es Salaam kuongoza kunaweza kuchangiwa na idadi ya watu waliopo pia uchumi wake ni mkubwa ukilinganisha na kanda nyingine lakini hata starehe hii ni sehemu inayoongoza kwa kuwa na baa nyingi nadhani kuliko eneo lingine lolote,” amesema mmoja wa watumishi katika kampuni ya uzalishaji bia ambaye hakutaka kuandikwa jina.
Akiwa mtu wa masoko katika kampuni hiyo, anadai ubunifu ni moja ya jambo ambalo limekuwa likiwavutia watu wengi kuendelea kutumia kinywaji hicho.
“Unajua hii ni biashara kila mtu ana ubunifu wake, wengine watakuja na zawadi chini ya kizibo, wengine kunywa kistaarabu, wengine watakuja na hili hizi zote zinavuta wateja kuendelea kutumia bidhaa zako,” amesema.
Hilo linasemwa wakati ambao matumizi ya stempu za kielektroniki (ETD) inatajwa kuwa moja ya sababu inayofanya bidhaa za vinywaji kuongezeka kutokana na kutambuliwa kirahisi.
Suala hilo linatajwa pia kuwa moja ya jambo linaloweka urahisi katika ukusanyaji wa bidhaa za vinywaji.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amesema: “katika kila chupa kuna kodi ya ushuru wa bidhaa ambayo inatozwa na kuchangia kwenye kapu kuu la Taifa,” alijibu kupitia ujumbe mfupi wa maandishi.
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Goodhope Mkaro amesema ukuaji wa uzalishaji wa bidhaa hizo unachochewa na kukua kwa idadi ya watu inayoongeza mahitaji yake sokoni.
“Kitu kama pombe huwa inatumika kwa tabia bila kujali bei ndiyo viburudisho vinapatikana kirahisi hata bei ikipanda watatumia,” amesema Dk Mkaro.
Amesema kutokana na mazoea bidhaa hizo zimekuwa zikitumika katika maeneo mbalimbali ikiwamo sherehe zote au msiba licha ya kutokuwapo kwa ongezeko la wazalishaji.
“Wazalishaji ni walewale tunawaona, lakini wamekuwa wakijitahidi kwenda sambamba na ongezeko la mahitaji kwa sababu ni bidhaa ambazo hazinunuliwi kwa msimu, kitu kama soda na bia kuna mtu akimaliza kula anasema nipate soda nishushie,” amesema.
Amesema tabia hiyo ndiyo iliyowafanya watu kuendelea kuvihitaji zaidi vinywaji hiyo jambo ambalo pia linachochea ukuaji wa uchumi kutokana na mauzo kuongezeka sambamba na uzalishaji.
“Kichocheo kingine ni ubunifu kwa sababu bidhaa hizi hazihitaji kutangazwa sana kutokana na kujulikana kwake lakini ule ubunifu wa kuja na soda labda isiyokuwa na sukari, sijui soda kwa watu wanaofanya diet imeongeza kiwango cha matumizi,” amesema.
Mtaalamu wa Uchumi, Lameck Mlay amesema kuwapo kwa ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hizo inamaanisha kukua kwa mahitaji na ongezeko la matumizi ya vimiminika.
Amesema ukuaji huo pia unaonekana kwa sababu bidhaa hizo ndiyo zilizoweza kufika sokoni kwa urahisi hata katika maeneo ya vijijini zinapatikana.
“Ili kuendelea kushuhudia ongezeko hili ni vema Serikali kuendelea kuwa karibu na wazalishaji ili wasije kurudishwa nyuma kwa changamoto zozote na badala yake lita ziongezeke. Kadri uzalishaji unavyokua ndivyo mchango wake kwenye uchumi unaongezeka,” amesema.
