Ramadhan Chomelo kutimkia Depsas Enerji

KUNA asilimia kubwa kwa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Konya Amputee inayoshiriki Ligi Kuu ya Walemavu Uturuki, Ramadhan Chomelo akatimkia Depsas Enerji ya nchini humo.

Kama atafanikiwa kukamilisha uhamisho huo basi inaweza kuwa msimu wake wa nne mfululizo kuitumikia Ligi ya Uturuki akiujiunga nayo msimu wa 2022 alipotokea Tanzania.

Chanzo cha kuaminika kililiambia Mwanaspoti kuwa tayari Chomelo amemalizana na chama lake la zamani hivyo yuko kwenye hatua za mwisho kujiunga na Depsas Enerji inayoshirki pia ligi kuu.

Kiliongeza kuwa sababu ya kuondoka kwa kiungo huyo ni maslahi kwani chama lake la zamani liliweka ofa ndogo iliyochangia nyota huyo kutimka.

“Kuanzia sasa huenda akatangazwa wamempa mkataba aupitie. Ilikuwa jana Jumapili nafikiri ofa imemfanya Chomelo avutiwe nao, ataangalia masharti kama ataendena nao basi atasaini na kuibukia huko,” kilisema chanzo hicho.

Msimu wake wa kwanza (2022/23) alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na kutoa asisti 16, huku msimu wa 2023/24 akicheza mechi 21 na kufunga manne na kutoa asisti tisa. Msimu uliopita aliweka kambani mabao matano na kutoa asisti 11.